HabariSiasa

BBI: Raila awarai viongozi 'watapike nyongo'

February 25th, 2020 2 min read

NDUNGU GACHANE na GEORGE SAYAGIE

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga amewatetea viongozi wanaodaiwa kueneza uchochezi katika mikutano ya hadhara ya kuhamasisha umma kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI).

Akizungumzia jinsi baadhi ya viongozi wamemshambulia Seneta wa Narok Ledama ole Kina kuhusu matamshi yake ya wikendi, Bw Odinga alisema mojawapo ya umuhimu wa mikutano hiyo ni kuwapa watu nafasi ya kueleza yaliyo moyoni mwao.

“Nimesikia viongozi wakisema kuna matusi hapa na pale, lakini ningependa kuwaambia hiyo ndiyo jinsi ya kuweka msingi bora kwa nchi hii. Hakuna mtu amekatazwa kusema jambo lolote linalomkera pamoja na jamii yake. Acheni kila mtu atapike nyongo na azungumze kwa uwazi ili tujenge Kenya mpya,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika Kanisa Katoliki la St Joseph the Worker Mumbi, Kaunti ya Muranga wakati wa mazishi ya Bw Joseph Irungu ambaye ni babake Seneta Irungu Kangata.

Kaunti asili za Wamaasai ni Narok na Kajiado. Wakazi wa Samburu pia wana uhusiano wa karibu wa maumbile na tamaduni na jamii ya Maasai.

Kikatiba, Mkenya yeyote huruhusiwa kuwania wadhifa wa kisiasa katika eneo lolote nchini bila kujali kabila lake.

Hapo Jumatatu Bw Ole Kina alitarajiwa kufika katika ofisi ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) mjini Narok kuandikisha taarifa kuhusu matamshi yake yaliyoonekana kulenga zaidi jamii ya Kipsigis.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa DCI katika Kaunti ya Narok Mwenda Ethaiba alisema uchunguzi huo unagusia matamshi ya Bw ole Kina ambayo yanaweza kuchochea fujo, lakini seneta huyo hakufika katika ofisi yake na aliomba apewe siku nyingine.

Kamishna wa Kaunti ya Narok, Samuel Kimiti naye alisema kamati ya usalama ya Kaunti ya Narok haitakubali mwanasiasa yeyote kutumia mikutano kusambaza chuki.

“Haijalishi unatoka kaunti gani lakini lazima kila mmoja afuate sheria. Tunahitaji amani ili tuishi pamoja kwani uchochezi unaweza kusababisha vita,” akasema kamishna huyo.

Kufuatia matamshi hayo, wandani wa Naibu Rais William Ruto walishambulia sana mikutano ya BBI wakisema matamshi ya Bw ole Kina ni dhihirisho kwamba lengo la BBI ni kugawanya nchi kuliko kuleta umoja.

Naibu Rais alitishia hata kutumia mamlaka yake kuzima mikutano hiyo, licha ya kuwa Rais Uhuru Kenyatta anaunga mkono BBI kama mpango ambao utasaidia kuleta umoja na amani nchini.

Jumatatu, Bw Odinga alisema kila mtu yuko huru kujieleza: “Mtu yeyote anaweza kujieleza. Tuna dawa ya kuwatibu,” akaeleza.

Wakati huo huo, waziri huyo mkuu wa zamani alisisitiza kwamba mchakato wa BBI haulengi kumwundia yeye nafasi ya urais na kumpa Rais Kenyatta wadhifa wa Waziri Mkuu ifikapo mwaka wa 2022 jinsi inavyodaiwa na wakosoaji wake.

“Hatutaki kumharibia mtu yeyote maazimio yake ya urais. Kila mtu asubiri hadi wakati utakapofika kumenyana na washindani wengine. Huu ni wakati wa kuleta umoja katika nchi yetu,” akasema.

Naye Gavana wa Muranga Mwangi Wa Iria alikashifu viongozi wanaoingiza siasa katika suala la BBI badala ya kutoa mapendekezo yao.

“Wanapotezea Wakenya muda kwa mambo ya upuuzi. Kama viongozi hawatatoa mchango wao, maeneo yao hayatanufaika wakati marekebisho ya katiba yatakapofanywa,” akasema gavana huyo.

Wandani wa Dkt Ruto waliokuwepo kwenye mazishi hayo pamoja na Bw Odinga, wakijumuisha Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, Mbunge wa Gatundu Moses Kuria, Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, walitumia nafasi hiyo kumsuta Bw Odinga ana kwa ana wakimwambia BBI inalenga kumnufaisha yeye kisiasa.

Walimkashifu pia kwa kutetea watu ambao wanatoa matamshi yanayoweza kugawanya nchi kikabila.