Habari

BBI: Rais afokea 'Tangatanga'

November 23rd, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta amewakemea wanasiasa wanaopinga ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) hata kabla ya kutangazwa rasmi akiwafananisha na wajinga wasiofahamu wanachofanya.

Akizungumza Ijumaa saa chache baada ya mwenyekiti wa jopokazi hilo, Yusuf Haji, kutangaza kuwa kamati yake itawasilisha ripoti hiyo kwake Jumanne ijayo, Rais Kenyatta alishangaa kwa nini wanasiasa hao wamekuwa wakiipinga ilhali hawajaiona.

“Kuna hawa watu wanaosema hawataki BBI ilhali hawajaona yaliyomo ndani yake. Hawa ni wajinga kwa sababu wanapinga kile ambacho hawajui,” Rais alisema alipoongoza hafla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Kibabii, kaunti ya Bungoma.

Aliongeza: “Tunawapeleka watu shule ili waweze kufundishwa kusoma. Kwa hivyo, tunapaswa kutumia muda wetu, tuisome pamoja na kuibuka na mambo mazuri ambayo yanaweza kuboresha nchi hii, ambayo yanaweza kufanya taasisi zetu kushirikisha wote na kuleta umoja nchini.”

Rais Kenyatta alithibitisha kuwa ataipokea ripoti hiyo Jumanne alivyotangaza Bw Haji.

“Nimewaambia kuwa wako huru kuileta Jumanne. Nawahakikishia kuwa baada ya kuipokea, binafsi nitaisoma kabla ya kuitoa kwa Wakenya wote,” alisema huku akiwataka wanasiasa kukoma kuingiza siasa katika ripoti hiyo.

Tangu jopo kazi hilo likamilishe kuandaa ripoti hiyo Oktoba 2019 wabunge kutoka mrengo wa ‘Tangatanga’ katika chama cha Jubilee wamekuwa wakitisha kuipinga iwapo itapendekeza mageuzi ya katiba ili kubuniwa kwa nafasi zaidi za uongozi.

Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, viongozi hao wameapa kupinga ripoti hiyo ikiwa itapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa uongozi wa ubunge kwa kubuniwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Kwa upande mwingine, wanasiasa wanaoegemea mrengo unaounga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakiipigia debe ripoti hiyo, wakisema imesheheni “mambo mazuri ya kuboresha nchini katika nyanja zote.”

Kukataa

Ijumaa, wanachama wa ‘Tangatanga’ walisisitiza kwamba watakataa ripoti hiyo ikiwa haitakuwa ya kufaidi raia.

Wakihutubu katika ukumbi wa Bomas walipohudhuria sherehe ya kumpongeza Macdonald Mariga kwa kuibuka wa pili kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra, wabunge hao walisema wataikataa bungeni ikiwa lengo lake ni kufaidi wachache.

Hata hivyo Ijumaa, Bw Haji alipuuzilia mbali yale aliyoyataja kama uvumi kuhusu yaliyomo katika ripoti hiyo, huku akivitaka vyombo vya habari kukoma kusambaza habari alizotaja kuwa ‘feki’.

“Ripoti kama hizi za kupotosha zinalenga kuwakanganya na kuleta migawanyiko miongoni mwa Wakenya hasa zinaposambazwa katika mitandao ya kijamii. Huu ni wakati ambapo kuna muafaka kuhusu haja ya kuwepo kwa uwiano na utangamano wa kitaifa,” akasema akiwa ameandamana na baadhi ya wanachama 14 wa jopokazi hilo.

“Tunawaomba wanahabari na umma kwa jumla kuwasiliana nasi ili wathibitishe ripoti, taarifa na barua mbalimbali zinazodaiwa kutoka kwa jopokazi la BBI,” Bw Haji akaongeza.

Mwenyekiti huyo alisema walipokea maoni na mapendekezo kutoka kwa zaidi ya Wakenya 7,000 wa matabaka mbalimbali katika vikao walivyoandaa katika kaunti zote 47.

Jopokazi hilo liliundwa baada ya muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018, kupendekeza njia za kupata suluhu kwa mambo mbalimbali ambayo huleta machafuko kila baada ya uchaguzi mkuu.

Baadhi ya masuala ambayo lilishughulikia ni pamoja na; ukabila, baadhi ya watu kuhisi kutengwa serikalini, njia za kukomesha ufisadi, namna ya kuimarisha mfumo wa uchaguzi, kuimarisha ugatuzi, usawa, miongoni mwa mengine.

 

Na CHARLES WASONGA,DENNIS LUBANGA na COLLINS OMULO