Siasa

BBI: Ruto achangamkia ahadi ya Raila

November 10th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amechangamkia ahadi iliyotolewa na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwamba ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) itafanyiwa mabadiliko kujumuisha matakwa ya jamii za wafugaji.

Ni kufuatia ahadi hiyo ya Bw Odinga ambapo viongozi kutoka jamii za wafugaji Jumatatu walitangaza kuwa watainga kikamilifu ripoti hiyo ya BBI ambayo ilizinduliwa mwezi jana.

Kupitia ujumbe katika twitter Dkt Ruto alisema mapendekezo ya jamii ya wafugaji kuhusu masuala mbalimbali yaliyoko katika ripoti ya BBI ni yenye manufaa..

“Hakikisho lililotolewa hadharani kwamba ripoti ya BBI itafanyiwa marekebisho ili kuhujumisha masuala yaliyoibuliwa na jamii za wafugaji na hatua nzuri inayotoa matumaini ya kupatikana kwa muafaka kuhusu suala hilo,” akasema.

Dkt Ruto akaongeza: “Baada ya ombi hilo na mengine kukubaliwa, kun matumaini kuwa mjadala usiobishaniwa utafikiwa.

Wakiongozwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani na Katibu wa Kundi la Wabunge wa Jubilee Aden Kayna viongozi hao walitoa tangazo hilo baada ya kukutana na Bw Odinga katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

“Ningependa kuthibitisha kuwa tumejadili suala hili na kuamua kuwa tutaunga mkono BBI kikamilifu. Tungependa kushukuru Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kututengea nafasi maalum katika suala hili la kitaifa,” Bw Yatani akawaambia wanahabari baada ya mkutano wa viongozi wa jamii za wafugaji na Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa ODM alikubaliana na ombi la viongozi hao kwamba Hazina ya Kupiga Jeki Maendeleo katika maendeleo yaliyotengwa (Equalization Fund) idumishwe kwa miaka 20, kuundwe Mamlaka ya Uuzaji Bidhaa za Mifugo (Livestock Marketing Authority) na kwamba mgao wa fedha kwa kaunti usitolewe kwa misingi ya idadi ya watu.

“Masuala hayo matatu yaliyoibuliwa na jamii za wafugaji zitashughulikiwa ipasavyo. Kamati ya kiufundi itaketi chini na kuyachunguza kwa lengo la kuyajumuisha katika miswada itakayoandaliwa kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya BBI,” akasema Bw Odinga.

Aliongeza kuwa ni muhimu kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na jamii za wafugaji ili utajiri wa maeneo hayo yanaweza kufaidi wakazi wa huko.

“Maeneo ya wafugaji yana utajiri mkubwa wa rasilimali kando na vivutio vya utalii na shughuli nyinginezo za kibiashara. Ustawishaji wa miundo msingi katika maeneo hayo ni muhimu kwa sababu yalitengwa kimaendeleo kwa miaka mingi,” akasema Bw Odinga.

“Tunapasa kuongea lugha moja kwa sababu kila Mkenya ni sawa na mwenzake,” akaongeza.

Bw Yatani alisema viongozi wa jamii za wafugaji wataunda kamati ya kiufundi ambayo itashirikaina na ile ya BBI kuhakikisha kuwa masuala hayo yanajumuishwa katika mswada wa mwisho.

Masuala ambayo yalitambuliwa hapo awali lakini viongozi hao wa jamii za wafugaji waliamua kuyaweka kando ni kama vile kupandisha hadhi kwa Seneti kuwa Nyumba ya Juu na kuondolewa kwa pendekezo la kubuniwa kwa Tume ya Huduma za Afya (HSC).

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto alisema masuala yaliyoibuliwa na jamii wafugaji, makundi ya kidini, wanawake, Seneti na wadau wengine yanapasa kujumuishwa ndani ya BBI.

“Ni kinaya kwamba tunataka kuifanyia marekebisho katiba ilhali tunakataa kuifanyia marekebisho mapendekezo kwene ripoti. Hamna maana kujenga ukuta wa kuwafugia nje wengine huku tukijifanya kuwa tunajenga madaraja,” akasema.