MakalaSiasa

BBI: Sababu ya ODM kutaka muda uongezwe

December 17th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

ODM inaunga mkono kuongeza kwa muda wa jopo la maridhiano (BBI) kwa ajili ya kukushirikisha umma katika mpango wa utekelezaji wa ripoti yake iliyozinduliwa majuma mawili yaliyopita huku ikisisitiza kuwa mchakato huo sharti uendelee kuongozwa na wananchi.

Vile vile chama hicho Jumanne kilisema kuwa kinaunga mkono mapendekezo kwenye ripoti hiyo kwani yanawakilisha misimamo yake kuhusiana masuala mbalimbali yaliyotajwa katika muafaka wa maelewano kati ya kiongozi wake, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta Machi 9, 2018.

“Kwa mfano, tumekuwa tukitetea kuimarishwa kwa ugatuzi, ufikiaji wa usawa wa kijinsia, uimarishwaji wa vita dhidi ya ufisadi na kuimarishwa kwa uwezo wa vijana wetu na tunaridhika kuwa ripoti hiyo imeshughulikia haya,” Katibu Mkuu Edwin Sifuna akawaambia wanahabari baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho uliofanyika katika mkahawa wa Convent International, Nairobi.

Aliandama na wabunge Opiyo Wandayi (Ugunja), Florence Mutua (mbunge mwakilishi wa Busia), Denitah Gati (Mbunge Maalum), Anthony Oluoch (Mathare) Onyango K’Oyoo (Muhoroni).

“Tunalipongeza jopo la BBI na umma kwa kufanya kazi nzuri,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Sifuna alisema mkutano huo wa NEC ulitambua sehemu kadhaa katika ripoti hiyo ambayo zinapasa kuimarishwa zaidi.

Alidokeza kuwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo ulioongozwa na Bw Odinga, waliwasilisha mapendekezo zaidi hasa yanayolenga kuwafaidi wanawake, watu wanaoishi na ulemavu na vijana.

Japo Bw Odinga alihudhuria mkutano huo, alikataa kuongea na wanahabari, na kuacha jukumu hilo kwa Bw Sifuna.

“Kwa mfano, kwa kuwa BBI imependekeza msamaha wa ushuru, wa kipindi cha miaka saba, kwa vijana wanaoendesha biashara, viongozi wa chama chetu wanahisi kwamba nafuu hiyo pia ipanuliwe ili iweze kuwafaidi vijana ambao wameajiriwa na wale ambao wanajishughulisha na michezo na fani mbalimbali za sanaa,” akasema Bw Sifuna.

ODM pia inataka mageuzi katika sekta ya elimu yafanywe kwa lengo la kupunguza gharama ya elimu ya juu ili vijana wasibeshwe mizigo ya mikopo baada ya kuhitimu kutoka vyuo mbalimbali vya mafunzo.

Bw Sifuna aliwataka viongozi na wanachama wa ODM kote nchini kutumia msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya kuwahamisisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya BBI “ili waweze kuilewa zaidi.

Kauli ya ODM inajiri siku chache baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuongeza muda wa kuhudumu wa wanachama wa jopo la BBI.

“Hatua hii itatoa nafasi kwa jopo la BBI kuongoza ushirikishwaji wa umma katika kuichambua ripoti hii na kuainisha mapendekezo ya ripoti yake kwa namna ambayo itaweza kutekelezwa kwa mpangilio mzuri,” akasema msemaji wa Ikulu Bi Kanze Dena kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi.

Haikujulikana ni kwa muda gani jopo hilo la BBI litaendelea kuhudumu lakini kulingana na ripoti yake utekelezaji wake utafanywa ndani ya kipindi cha miezi 18.

Hatua hiyo hata hivyo, imeibua hisia mseto miongoni mwa wanasiasa na viongozi wa kidini.

Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alipinga kuongezwa muda wa jopo hilo la watu 14 linaloongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji akipendekeza uteuzi wa kamati ndogo ya wataalamu kuchambua ripoti hiyo.

Pendekezo sawa na hilo pia lilitolewa na wabunge na maseneta za zamani kutoka Mlima Kenya ambao walisema wataalamu hao wanafaa kuanisha sehemu za ripoti hiyo ambazo zinapasa kutekelezwa kupitia kura ya maamuzi au bunge.

Nalo Baraza Kuu la Kiislamu Nchini (Supkem) lilitaka jopo hilo lipanuliwa ili kujumuisha wanachama zaidi, haswa vijana.

Kwa upande wake, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alidai kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga waliongeza muda wa kuhudumu kwa BB kwa sababu ripoti iliyozinduliwa ilikuwa “feki”.

“Ripoti asilia ilipendekeza kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka. Lakini kutokana na shinikizo kutoka kwa umma pendekezo hilo lilioondolewa. Sasa wameongeza muda wa BBI ili itoe ripoti itakayoendana na matakwa yao,” akasema Bw Kuria.