Siasa

BBI: Uhuru na Raila walegeza msimamo

November 10th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wanafanya kazi ya ziada ili kuzima uasi unaoibuka katika azima yao ya kubadilisha katiba baada ya makundi kadhaa kukosoa baadhi ya mapendekezo ya ripoti ya mwisho ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Ingawa wiki jana, walipokutana na wabunge mjini Naivasha walisema ripoti hiyo haingebadilishwa kabla ya kura ya maamuzi, wameanza kukutana na makundi yaliyolalamika kuwasikiliza na kuahidi kwamba maoni yao yatazingatiwa.

Jana, Bw Odinga alikutana na viongozi kutoka jamii za wafugaji ambao wiki jana walilalamika kuwa maslahi ya jamii zao hayakuwa yamezingatiwa.

Bw Odinga alisema maoni ya viongozi hao hasa kuhusu hazina ya uzawazishaji, kubuniwa kwa mamlaka ya kusimamia mifugo na ugavi wa mapato ya serikali yatazingatiwa.

Viongozi hao wakiwemo, wabunge, magavana, mawaziri na makatibu wa wizara kutoka jamii za wafugaji walishukuru Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kukubali maoni yao.

Leo, waziri mkuu huyo wa zamani na Rais Kenyatta walikukutana na magavana wanaokutana Naivasha kusikiliza malalamiko yao kuhusu ripoti hiyo.

Wiki jana, Bw Odinga alikutana na magavana hao jijini Nairobi kusikiliza malalamishi yao kuhusu ripoti hiyo.Wiki jana, Rais Kenyatta alikutana na baadhi ya viongozi wa kisiasa waliozua maswali kuhusu ripoti hiyo. kabla ya kuondoka nchini kwenda Italia.