Habari Mseto

BBI: Wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani kurudishwa

November 27th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RIPOTI ya Jopo la Maridhiano imependekeza kubuniwa kwa wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni.

Wadhifa huo utashikiliwa na mgombeaji wa urais ambaye ataibuka wa pili katika uchaguzi wa urais kwenye uchaguzi mkuu na atakuwa kiongozi wa chama au muungano wa vyama vinavyowakilishwa bungeni lakini ambavyo havijawakilishwa serikalini.

Na kulingana na muhstasari wa ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa rasmi kwa Rais Uhuru Kenyatta jana katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi huyo wa upinzani pia atahudumu kama mbunge.

‘Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni atateua baraza lake la Mawaziri Butu ambao wataendesha kazi ya kupiga msasa utendakazi wa mawaziri wa serikali,’ inasema ripoti hiyo.

Pendekezo hilo la BBI linaambatana na lake Naibu Rais William Ruto mwezi Februari mwaka huu alipotoa hotuba katika kituo cha Chatham House jijini London, Uingereza.

‘Binafsi napinga pendekezo la kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka. Badala yake ningependekeza kurejeshwa kwa wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni ambaye kazi yake itakuwa ni kupiga darubini utendakazi wa serikali,’ akasema.

Kurejeshwa kwa wadhifa huu kunarejesha kumbukumbu ya hali ilivyokuwa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya kisiasa.

Mwanasiasa wa kwanza kushikilia wadhifa huo aliyekuwa ni marehemu Jaramogi Oginga Odinga kwa kuwa chama chake cha Ford Kenya ndicho kilikuwa na wabunge wengi (31) miongoni mwa vyama vya upinzani wakati huo.

Baada ya kifo cha Jaramogi, wadhifa huo ulishikiliwa na aliyekuwa makamu wa Rais Christopher Wamalwa Kijana ambaye alitwaa wadhifa wa kiongozi wa Ford Kenya.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 1997 wadhifa wa kiongozi rasmi wa upinzani ulishikiliwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa misingi kuwa chama chake cha Democratic Party (DP) ndicho kilikuwa na wabunge wengi.

Na baada ya uchaguzi mkuu wa 2002 ambapo Mzee Kibaki alishinda urais, kiti hicho kilimwendea Rais wa sasa Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa kiongozi wa Kanu.

Wadhifa huo uliondolewa baada ya kuzinduliwa kwa Katiba ya sasa mnamo 2010.