Habari MsetoSiasa

BBI: Wadhifa wa ugavana Nairobi hatarini

November 27th, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

KAUNTI ya Nairobi huenda ikakosa kuwa na gavana kama kiongozi wake mapendekezo kwenye ripoti ya jopokazi la Building Bridges Initiative (BBI) yatapitishwa.

Ripoti ya jopokazi la BBI, iliyokabidhiwa rasmi Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, haisemi lolote kuhusu nyadhifa za gavana na seneta kwa jiji kuu hilo nchini.

Jopokazi hilo limeeleza tu kwamba, kaunti hiyo itakuwa na wadi zitakazoongozwa na madiwani pamoja na wabunge watakaochaguliwa katika maeneobunge.

Hata hivyo, ripoti hiyo nusura ipendekeze kufutiliwa mbali kwa serikali ya kaunti.Ripoti hiyo inatarajiwa kuzinduliwa hadharani na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM leo katika Bomas of Kenya ambapo wageni 4, 700 wamealikwa kuhudhuria sherehe hiyo.

Kaunti ya Nairobi ina wadi 85 zinazowakilishwa na madiwani ambao ni sehemu ya Bunge la Kaunti ya Nairobi pamoja na maeneobunge 17 yanayowakilishwa na wabunge na maseneta.

Kaunti hiyo kwa sasa, inaongozwa na gavana Mike Sonko aliyechukua hatamu mnamo Agosti 2017 kutoka kwa aliyekuwa gavana wa kwanza kaunti hiyo Dkt Evans Kidero.

Aidha, ripoti hiyo imependekeza Nairobi kutunukiwa Hadhi Maalum kama Jiji Kuu nchini na kituo kikuu cha Umoja wa Mataifa na uwakilishaji mwingineo wa kidiplomasia.

Hii inamaanisha kuwa serikali hiyo ya kaunti huenda sasa ikawa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu na wala sio kuongozwa na gavana jinsi ambavyo imekuwa kwa kipindi cha miaka saba iliyopita.

Nairobi ni makao makuu mashirika kadha ya Umoja wa Mataifa.