Habari MsetoSiasa

BBI: Wakenya kupata fursa kukagua mali ya rais na wakuu serikalini

November 27th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

WAKENYA watapata fursa ya kujua na kutathmini utajiri wa maafisa wote wa umma akiwemo rais ikiwa mswada uliopendekezwa na ripoti ya jopokazi la Building Bridges Initiative (BBI) utapitishwa.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa jana, maafisa wa umma watatakiwa kuweka wazi fomu za kutangaza mali yao ili kuruhusu wananchi kuziona na kuzikagua.A

idha, kulingana na ripoti hiyo iliyokabidhiwa rasmi jana Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Orange Democratic Momevement (ODM) Raila Odinga, itakuwa ni marufuku kwa wafanyakazi wa umma kufanya biashara na serikali.

Hatua hii ni miongoni mwa juhudi za kubatilisha mapendekezo ya Tume ya Ndegwa yaliyotolewa mnamo 1971 kuhusiana na huduma ya umma.

Mapendekezo mengineyo katika ripoti hiyo inayodhamiria kukomesha mfumo unaoendeleza ufisadi na ubaguzi nchini, ni pamoja na kuwatunukia kijisehemu cha mali itakayonusuriwa, watu ambao watatoa habari muhimu kuhusu njama za ufisadi.

Katika hatua ya kupambana na ufisadi, watu watakaofichua habari muhimu kuhusu mikataba ya ufisadi watapokea asilimia 5 ya mapato yatakayookolewa ili kuwatia moyo wananchi zaidi kufunguka kuhusu njama za ufisadi.

Kando na zawadi, ripoti ya BBI inapendekeza kubuniwa kwa mikakati maalum ya korti itakayowezesha kutoa ulinzi na usalama kwa wale watakaofichua habari muhimu kwa manufaa ya taifa.

Miongoni mwa watakaopata ulinzi huo ni wanaofichua habari muhimu pamoja na mashahidi kuhusu masuala hatari kama vile mipango ya ugaidi, njama hatari za uhalifu kibiashara na ufisadi kwa jumla.

Kuifanya Kenya kuwa taifa dijitali asilimia 100 kwa kutekeleza kidijitali huduma zote za serikali ikiwemo michakato, mifumo ya malipo na kuhifadhi rekodi, ni miongoni mwa mabadiliko muhimu yatakayokea iwapo ripoti ya BBI itafanikishwa.

Serikali vilevile, kupitia ripoti ya BBI inanuia kuimarisha imani ya raia katika Idara ya Mahakama kwa kutambua kanuni kuu za Katiba zizojumuisha kugawanya mamlaka baina ya matawi ya Serikali pamoja na kuwajibika kwa raia.

Kuambatana na mswada huo, uhuru wa Idara ya Mahakama ni sharti ulindwe kama kanuni kuu ambapo tawi hilo la serikali pia ni sharti liwajibike kwa Wakenya.

Kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kupiga vita ufisadi, jopokazi la BBI limependekeza kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari katika utendakazi wake.

Vyombo vya habari kwa upande wake vinatakiwa kuhakikisha vinajiepusha na kutatiza utoaji huduma kwa wananchi kupitia uchapishaji wa habari za uongo pamoja na kuwaharibia sifa watu wengine.