Habari MsetoSiasa

BBI: Wanasiasa watatimiza ahadi hizi?

November 28th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA Na MARY WANGARI

RIPOTI ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), ilizinduliwa rasmi Jumatano katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi katika hafla iliyowaleta pamoja viongozi wa kisiasa wa vyama na mirengo mbalimbali.

Wote waliopewa nafasi ya kuhutubu waliisifu ripoti hiyo wakisema wataiunga mkono ili kusulushisha matatizo ambayo yanakumba nchi kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo, ikizingatiwa kuwa mjadala kuhusu ripoti hiyo utafanyika wakati wanasiasa wanapojiadaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022, swali ambalo Wakenya wanajiuliza ni ikiwa wanasiasa watatimiza ahadi yao ya kuweka maslahi ya nchi mbele, au walikuwa wakitoa ahadi hewa kisha wageuze mjadala huo kutimiza malengo yao ya kibinafsi.

Rais Uhuru Kenyatta alikiri kuhusu unafiki wa wanasiasa alipowataka wawe waaminifu badala ya kujifanya wangwana wanapozungumza hadharani, na baadaye kuendeleza vitendo vya kugawanya Wakenya.

“Tatizo letu kama nchi ni wanasiasa. Sisi ndio tunafanya nchi kuoza. Tatizo letu ni kuwa mirengo ya wanasiasa inasababisha migawanyiko na kuzua taharuki ambayo huzaa ghasia. Ni lazima tufanye jambo kuunganisha Wakenya. Tukomae sasa ili tuache kugawanya Wakenya,” Rais Kenyatta akasema kwenye hotuba yake.

Aliwataka wanasiasa kuvunja mirengo ya kisiasa ya ‘Tangatanga’, ‘Kieleweke’, ‘Inua Mama’ na ‘Embrace’ ambayo imekuwa na misimamo mikali kuhusu uchaguzi wa 2022 na BBI.

“Ripoti hii sio kuhusu Uhuru, Ruto, Raila, Kalonzo, Mudavadi, Wetangula na wale wengine. Ni kuhusu wewe na mimi na ni kuhusu Kenya,” Rais Kenyatta alisema na kuwataka Wakenya wote kujisomea ripoti hiyo.

Naibu Rais William Ruto pia alieleza uwezekano wa wanasiasa kutumia ripoti hiyo kujifaidi kibinafsi aliposema kuwa haifai kutekwa na wanaotaka vyeo, mbali inafaa kutumiwa kuimarisha maisha ya Wakenya.

“Mjadala huu haufai kutekwa na wanasiasa. Usiwe ni kuhusu nani atachukua cheo gani. Ripoti hii inafaa kulenga matarajio ya Wakenya wengi. Tukiendelea mbele, sote tunataka kuwa na mjadala wa wazi, wa kidemokrasia na unaoshirikisha kila mmoja ambapo hakutakuwa na maoni mazuri au duni,” alisema Dkt Ruto.

“Nina imani kwamba tuko na uwezo wa kuhakikisha ripoti hii imefaulu,” akasema Dkt Ruto ambaye awali alikuwa akipinga ripoti hiyo.

Ikizingatiwa Dkt Ruto na kundi lake la Tanga Tanga walikuwa wameapa kupinga ripoti hiyo, Wakenya wanasubiri kuona iwapo watatimiza ahadi waliyotoa kwa Wakenya jana.

Kinara wa ODM, Raila Odinga naye aliahidi kuwa ripoti hiyo haitaingizwa siasa za 2022.

“Ripoti ya BBI haihusu siasa za 2022 lakini inalenga kurekebisha makosa yaliyotokea kwenye chaguzi zilizopita na katika siasa. Tunataka Kenya iliyoungana. Tunataka kuona Wakenya wakishirikiana. Hili ndilo lengo la BBI,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi naye alisema ripoti hiyo ikitekelezwa itatoa suluhu kwa matatizo ya Kenya.

“Nina furaha kuwa huu ni wakati tunaoweza kutumia kurekebisha mambo. Ni matumaini yetu kuwa kila Mkenya atajisomea ripoti hii, na kuamua mwenyewe,” alisema.

“Tuwe wazi katika mjadala huu. Tudadisi na kujadili ripoti hii. Tujisomee wenyewe. Mjadala ushirikishe watu wote na tushawishiwe na wazo kwamba tutajenga Kenya bora,” aliongeza na kuomba suala la kudorora kwa uchumi lishughulikiwe huku ripoti ikijadiliwa.

Kulingana na Bw Mudavadi, mjadala haufai kuwa kuhusu nyadhifa za uongozi, mbali kuhusu jinsi ya kutatua matatizo yanayowakumba Wakenya.

Kulingana na seneta wa Kaunti ya Bungoma, Moses Wetangula, huu ni mwanzo wa ukurasa mpya kwa Kenya.

“Huu ni mwanzo ambao utafungua nafasi ya Wakenya siku zijazo wawe wakisoma katika historia yetu kuhusu ghasia za kisiasa. Natudadisi ripoti hii kwa makini na kurekebisha panapowezekana. Kwa kufanya hivi, tutakuza amani katika nchi yetu. Tusome ripoti hii vyema,” alisema Bw Wetangula.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka aliwahimiza Wakenya kuepuka hasira wanapojadili ripoti hii akisema ni mwanzo mpya kwa Kenya.

“Ripoti hii inaonyesha mwanzo wa Kenya mpya. Huu ni wakati wa kuunganisha Wakenya wala sio wa kukasirika kwa sababu hasira haitendi haki ya Mungu,” akaeleza Bw Musyoka.