Makala

TAHARIRI: Wenye maoni tofauti BBI wasitengwe

November 28th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

KUZINDULIWA rasmi kwa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) jana kunapaswa kuwa mwanzo mpya wa safari ya maridhiano ya kweli nchini.

Uzinduzi huo huenda ukaashiria mwanzo mpya kwa Kenya, ikiwa hotuba za kufana zilizotolewa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta zitatekelezwa.

Kwa muda mrefu, imekuwa kawaida kwa viongozi wa kisiasa kutoa ahadi na hakikisho mbalimbali kwa wananchi, lakini baadaye huwa wanazisahau.

Kwenye hafla hiyo, iliyofanyika katika Jumba la Bomas jijini Nairobi, Rais Kenyatta aliwasisitizia Wakenya kuhusu athari za siasa za migawanyiko, akieleza kuwa umoja ndiyo njia pekee itakayoiwezesha Kenya kupata ustawi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kwa undani, ripoti ya BBI inatoa mapendekezo mazuri ambayo huenda yakazika katika kaburi la sahau, migawanyiko ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.

Kauli ya Rais Kenyatta inawiana na zile zilizotolewa na kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto, ambapo wote walikubaliana kwamba ripoti hiyo inaashiria mapambazuko mapya ya kisiasa nchini.

Hata hivyo, huenda ahadi hizo zikakosa kutimizwa ikiwa kutakuwa na viongozi ama makundi yatakayotengwa kwenye mchakato wa utekelezaji wake.

Kwa mfano, ulikuwa mwanzo mbaya kwa ripoti hiyo baada ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen, kudai kwamba viongozi ambao wamekuwa wakitoa maoni tofauti kuhusu ripoti hiyo walitengwa. Ni hali iliyomkasirisha kiasi cha kushindwa kuhimili hasira zake.

Kando naye, baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa ‘Tanga Tanga’ walinukuliwa wakilalamika kwamba hafla hiyo ilionekana kudhibitiwa na wenzao wa mrengo wa ‘Kieleweke.’

Bila shaka, haya ni madai yenye uzito ambayo hayapaswi kuwepo kwenye shughuli muhimu kama hiyo.

Ni muhimu viongozi waelewe kuwa ni lazima kutakuwa na watu watakaokuwa na maoni tofauti kuhusu mapendekezoi ya ripoti hiyo.

Badala ya kutengwa ama kudharauliwa, maoni yao yanapaswa kuzua mjadala muhimu kuhusu njia bora za kutatua changamoto zinazotukabili.

Litakuwa kosa kubwa kuwatenga. Hayo yatakuwa maonevu ya wazi dhidi yao, ilhali wao no viongozi wanaowakilisha sehemu ya nchi hii.