Habari

BBI yalewesha wanasiasa

December 15th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANASIASA nchini wanaendelea kuzama katika mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI na kusahau masuala muhimu yanayokabili nchi.

Ingawa nchi inakabiliwa na changamoto ya janga la corona na kiuchumi, wanasiasa wengi wamefumbia macho masuala hayo wakiweka nguvu kusukuma BBI ambayo ikipita itakuwa imewasaidia wao na wakati huo huo kuongezea wananchi mzigo wa ushuru.

Wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Jamhuri mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alipatia BBI umuhimu mkubwa kuliko masuala mengine kama hali ngumu ya maisha inayowakabili Wakenya na mgogoro katika sekta ya afya.

Wabunge nao wamepatia mchakato huo wa BBI umuhimu mkubwa na kutaka utengewe pesa ili usikwame badala ya kushinikiza wizara hiyo kutoa pesa kwa serikali za kaunti zitoe huduma kwa umma.

“Kila siku wanasiasa wanazungumza kuhusu BBI, ambayo haijawapa wauguzi hata jambo moja waliloomba. Hadhi ya wahudumu wa afya ni muhimu zaidi ya BBI,” akasema Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi, (KUCO), Wachira Peterson hapo jana.

Mbali na janga la mgomo wa wauguzi, shule zinatarajiwa kufunguliwa katika muda wa wiki mbili zijazo baada ya kufungwa kwa miezi 10 kwa sababu ya corona, na serikali imelaumiwa kwa kutoweka mikakati ya kutosha kupokea wanafunzi.

Badala ya kushinikiza serikali itoe pesa kwa shule zijiandae kwa ufunguzi au kutoa pesa za kununua vifaa vya matibabu kukinga madaktari, wabunge wanashinikiza pesa za kufanikisha BBI.

Mnamo Ijumaa, mwenyekiti kamati ya bunge kuhusu bajeti Kanini Kega aliitaka Wizara ya Fedha kukabidhi Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) pesa inazohitaji kuiwezesha kukagua saini za kuunga mkono BBI.

Wanachofanya wanasiasa, ni kukashifu yeyote anayekosoa BBI kwa sababu wanatarajia kunufaika na nyadhifa zitakazobuniwa katiba ikifanyiwa mageuzi.

“Kwao, kila kitu kiko sawa kwa sababu BBI inawahakikishia vinono na vitamu,” asema mchanganuzi wa siasa Ndungu Wainaina.

Kulingana na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, BBI haiwezi kusitishwa hata ingawa nchi inakabiliwa na changamoto nyingi. Alisema jana kuwa wanaotaka mchakato wa kura ya maamuzi uahirishwe ili serikali ikabiliane na janga la corona wanajifanya kwa kuwa virusi hivyo haviwezi kuzuia BBI.

Hii ni licha ya idadi ya maambukizi kuongezeka na zaidi ya watu 1,500 kuuawa na virusi hivyo.

Bw Kiraitu alisema kwamba corona haiwezi kufanya BBI isitishwe kwa sababu kuna mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Viongozi wa kidini na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakihimiza Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kusitisha juhudi za kubadilisha katiba na kuelekeza pesa zilizotengewa mpango huo kulipa wahudumu wa afya na kuwanunulia vifaa vya kujikinga.

Bw Kiraitu alipuuza wito huo akisema kuwa huku mchakato wa kubadilisha katiba ukiendelea, serikali pia inakabiliana na changamoto zinazokumba nchi ikiwemo janga la corona.

“Kila wakati wa kubadilisha katiba ikiwemo tuliyopitisha 2010 huwa kuna matatizo makubwa lakini hayakuruhusiwa kusimamisha mageuzi,” alisema.

Alisema ingawa wale wanaopinga mageuzi wamekuwa wakiambia umma BBI ni mbaya kwa sababu ya maslahi yao ya kibinafsi hawatoi suluhu mbadala kwa masuala yanayoshughulikiwa kwenye mchakato huo.

“Jamii yetu imegeuzwa kuwa ukuta wa majuto wa Jerusalem ambako watu wetu wamefanywa kulalamika kila mara kuhusu matatizo lakini hakuna anayetoa suluhu. Shida ya ugatuzi ni pesa na suluhu ni BBI,” alisema Bw Kiraitu.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga anasisitiza kuwa hakuna kinachoweza kusimamisha reggae huku Rais Kenyatta akishikilia kuwa mchakato wa BBI ni zaidi muhimu kwa nchi.

Hapo jana wahudumu wa afya na wagonjwa walitoa mwito kwa Rais kushughulikia kwanza mgogoro wa sekta ya afya kabla ya kusukuma BBI.