HabariSiasa

BBI yatiliwa shaka baada ya marufuku ya Wako Amerika

November 19th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kumpiga marufuku aliyekuwa Mkuu wa Sheria, Bw Amos Wako kusafiri Amerika, imezua madahalo nchini baadhi ya Wakenya wakitilia shaka uadilifu wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) inayosubiriwa na ambayo alihusika kuandaa.

Wadadisi wa masuala ya  kisiasa na utawala wanasema kwamba hatua ya Amerika kwa mwanachama wa BBI, kamati ambayo mojawapo wa masuala iliyopatiwa jukumu la kushughulikia ni vita dhidi ya ufisadi, inafaa kutoa funzo kwa Wakenya.

Kwenye tangazo alilotoa Jumatatu, Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Amerika Mike Pompeo alisema Amerika ilimpiga marufuku Bw Wako, mkewe Flora Ngaira na mwanawe Julius Wako kwa kuhusika na ufisadi wa kiwango kikubwa.

Kulingana na Mhadhiri wa chuo kikuu cha Kenyatta Edward Kisiangani, kuna funzo ambalo Amerika ilitaka kutoa kwa Kenya kuhusu marufuku dhidi ya Bw Wako na watu wa familia yake wakati huu nchi inasubiri ripoti ya BBI.

Jopokazi hilo lilibuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kufuatia muafaka wao mnamo Machi 19 2018.

Bw Wako alikuwa Mkuu wa sheria kwa miaka 20 kati ya 24 ya utawala wa Rais Daniel Moi ambao maafisa wa serikali walihusishwa na ufisadi wa hali ya juu. Alilaumiwa kwa kuwalinda maafisa wakuu wa serikali waliohusishwa na kashfa za ufisadi akiwa mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala ya sheria.

Aidha, alilaumiwa kwa kubadilisha rasimu ya katiba ya Bomas ambayo ilipendekeza mageuzi makubwa na kuchelewesha Kenya kupata katiba mpya.

Wakenya kwenye mtandao walishangaa ni kwanini Tume ya Maadili na Ufisadi ya Kenya (EACC) haijawahi kumchunguza licha ya serikali ya Amerika kuwa na habari alihusika katika ufisadi.

“Seneta wa Busia Amos Waki amepigwa marufuku kuzuru Amerika kwa sababu ya ufisadi kwa sababu EACC haitamchunguza. Sababu ni kuwa Amos Wako ni mwanachama wa Jopokazi la Maridhiano (BBI) na mwandani wa karibu wa Raila Odinga,” @monda aliandika kwenye Twitter.

“Yaani mwanachama wa BBI Amos Wako ni kuhani wa ufisadi wa kimataifa na tunadanganywa kuwa BBI itatafuta suluhu la kudumu kuhusu ufisadi miongoni mwa masuala mengine,” alisema@thirinja.

Baadhi ya Wakenya walimtaka Bw Wako kujiuzulu kutoka kamati ya BBI na ripoti iliyoandaliwa na Jopokazi hilo kutupiliwa mbali ili ishughulikiwe na watu wenye maadili watakaokaguliwa na bunge.

“Raila na Uhuru mtaambia nini watu!?” aliuliza Mkenya kwenye Twitter. Kulingana na wakili Ahmednassir Abdullahi, kwa kumlenga Bw Wako, Amerika iliwaacha watu wasioweza kuguswa ambao wamehusika na ufisadi kwa sababu ya siasa.

Hii ilikuwa mara ya pili ya Amerika kumlenga Wako kuhusiana na madai ya ufisadi. Mnamo 2009, nchi hiyo ilionya kuwa ingemzuia kuizuru kwa sababu ya kuruhusu ufisadi Kenya.

Hata hivyo, alitisha kuishtaki na kuapa kuwa hakuwa na nia ya kukanyaga Amerika katika maisha yake.