Michezo

Beatrice Chepkoech aidhinishwa kutifua kivumbi cha Diamond League

July 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech Sitonik ni miongoni mwa mabingwa nne zaidi wa dunia wa hivi karibuni kuthibitishiwa kwamba watanogesha kampeni zijazo za Wanda Diamond League jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14, 2020.

Chepkoech, 29, atarejea katika ulingo uliomshuhudia akiweka rekodi yake ya dunia ya dakika 8:44.32 miaka miwili iliyopita.

Mbio za mwisho kwa Chepkoech kunogesha ni zile za World Athletics Indoor Tour zilizoandaliwa jijini Dusseldorf, Ujerumani mnamo Februari 2020.

Kivumbi hicho kilimpa fursa ya kusajili muda wa kasi zaidi dunia wa dakika 4:02.09 kufikia hatua ya mita 1,500.

Chepkoech aliambulia nafasi ya tatu na hivyo kuridhika na nishani ya shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya bara la Afrika mnamo 2015.

Anakuwa mwanariadha wa tano wa humu nchini kuthibitishwa kushiriki Diamond League baada ya bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake, Hellen Obiri na mfalme wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Conseslus Kipruto.

Wengine ni bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Chepng’etich Kipyegon na mfalme wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.