HabariMakalaSiasa

BEATRICE ELACHI: Ghasia ofisini zamsukuma kujificha chooni

September 10th, 2018 3 min read

Na PETER MBURU

GHASIA na vioja vilitawala bunge la Kaunti ya Nairobi Jumatatu, wakati madiwani walivamia Afisi ya Spika Beatrice Elachi kumlazimisha aondoke humo.

Madiwani hao ambao Ijumaa walimng’atua Bi Elachi kutoka kiti chake cha uspika walichukua hatua hiyo baada yake kuamkia afisini kama kawaida.

Bi Elachi anadaiwa kukimbia mahakamani Ijumaa kuzuia madiwani kumvua cheo chake hicho, japo viongozi hao wameshikilia kuwa maagizo ya korti hayaadhiri hatua yao kwani yalitoka wakiwa tayari wamemngatua.

Ilibidi maafisa wa usalama kuingilia kati purukushani hizo za Septemba 10, 2018. Picha/ Peter Mburu

Hali hii ya mvutano ndiyo ilisababisha vioja kutawala afisi ya spika huo wakati walipoingia kwa fujo, kwa muda fulani ikimlazimu kujificha chooni wakati walipoingia hadi anapoketi.

Japo kunao viongozi waliokuwa watulivu, baadhi yao walikuwa wakali na kumzomea Bi Elachi kuwa “amekuwa na roho mbaya” na kuwa katika hadhi yake hiyo milango yake haijakuwa wazi kuwahudumia.

“Huyu mama ana roho mbaya sana, kuna wakati nimekuja kutafuta msaada wake akaniweka hapo nje muda mrefu sana,” akasema mwakilishi mmoja.

Iliwabidi polisi pamoja na walinzi wa bunge kushika doria kali wakati wa purukushani hizo kumlinda Bi Elachi, huku mambo yalipochacha unga kiti chake kikatolewa nje katika visa vilivyotendeka kwa mazingira ya fujo tele.

Wanahabari pamoja na umma walimiminika katika ofisi za Bunge la Kaunti ya Nairobi kufuatilia matukio. Picha/ Peter Mburu

Lakini baadaye wanasiasa hao walitulizwa na viongozi wao, kiongozi wa wengi Abdi Guyo na wa wachache Elias Otieno kwa majadiliano katika afisi hiyo ya spika.

Wakati huo Bi Elachi bado alikuwa amejifungia chooni, huku baadhi ya viongozi wakijaribu kumshawishi atoke humo, hofu zikizidi kuwa aweza kufanya jambo baya.

Kiongozi wa Walio Wengi katika bunge hilo Bw Abdi Guyo Ijumaa alikana madai kuwa kuondolewa kwa Bi Elachi kunatokana na vita vikali ndani ya chama cha Jubilee.

Hiki ndicho kiti cha Spika. Kilitolewa nje ya ofisi na madiwani wenye hamaki waliomtaka Beatrice Elachi aondoke afisini mara moja. Picha/ Peter Mburu

Alisema kuwa Bi Elachi alipoteza fursa aliyopewa na rais kuhudumia wakazi wa jiji la Nairobi.

“Hoja hiyo ilitiwa saini na madiwani 112, ambapo 103 walipiga kura ya kumng’atua uongozini. Aliyewasilisha hoja aliwashawishi madiwani kuwa spika huyo alifaa kuondolewa. Mimi kama diwani, nilishawishika vya kutosha,” akasema.

“Lakini suala hili halifai kuonekana kama mvutano ndani ya Jubilee. Masuala yaliyoibuliwa dhidi ya Elachi yanahusu kila diwani. Ndio maana madiwani wengi waliona haja ya kumtoa.”

Ofisi ya Spika ilivunjwa kumfurusha Bi Elachi. Picha/ Peter Mburu

Bw Guyo alisema Elachi alialikwa kwa kikao cha pamoja kujadiliana kuhusu masuala hayo, lakini akakaidi kuhudhuria.

“Mwaka mmoja tangu tumchague, tukitoka kwa uongozi sawa, alikuja na ile akili ya jujiona akiwa na mamlaka zaidi kutuliko na wakati mwingi tulipomrai asuluhishe masula Fulani bungeni, alitupuuza,” Bw Guyo akaelezea.

Kudhihirisha mpasuko uliopo baina ya Elachi na madiwani bungeni, juhudi za vyama vikuu vya Jubilee na ODM kutaka kumwokoa dhidi ya shoka la madiwani ziligonga mwamba.

Kabla ya kung’atuliwa kwake, Elachi alikuwa amewalilia madiwani wakomeshe hatua za kupiga kura dhidi yake, akiwaomba wazungumze. Lakani wito wake ulifikia masikio yaliyotiwa nta.

Wakazi wa jiji nje ya ofisi za Bunge la Kaunti ya Nairobi wakati ghasia zilichacha mle ndani. Picha/ Peter Mburu

Katika kikao cha bunge hicho kilichohudhuriwa na madiwani wengi zaidi, walikuwa madiwani wa Jubilee waliokuwa kwa mstari wa mbele kumtaka naibu spika John Kamungu kuongoza mchakato wa kumng’oa Elachi ofisini.

Hoja hiyo ya kukos Imani naye pia iliwasilishwa na mwakilishi wa kaunti (MCA) wa chama cha Jubilee, Anthony Kiragu, idhibati kuwa hata tumaini la mwisho la kukomesha mchakato huo halikuwepo.

Cha kushangaza ni kuwa Elachi aliondolewa mamlakani tarehe sawa na ile alichaguliwa kuwa spika mwaka uliopita.

MCA wa matopeni alidai kuwa Elachi alikalia kiti cha uspika akijua kuwa bunge la kaunti ya Nairobi ilijaa ufisadi aliopaswa kutokomeza licha ya kuwa na mamlaka kuliko madiwani waliomchagua.

Kioja cha Bi Elachi kujificha kwa choo kilivutia umma kumtazama akitoka. Picha/ Peter Mburu

Kwa upande wake, Kiongozi wa Walio Wachache Peter Imwatok alisema, “Agizo la mahakama limepitwa na matukio. Linaelezea kuhusu kusimamisha mchakato ambao ulimalizika kabla yake.”

Akijitetea akiwa mjini Malindi, Elachi alisema kura dhidi yake ni kinyume cha sheria akitaja kuwa bado anafanya kazi yake ya uspika kwa kuzungumza na madiwani.

Alisema masaibu yake yanaongozw na Kiranja wa Bunge Jacob Ngwele, Kiongozi wa Wengi Abdi Guyo, na mwenzake wa Wachache Elisha Otieno.

Matatizo yalianZA Juni mwkaa huu Elachi alipowaita wapelelezi kuchugunza visa vya matumizi ovya ya fedha katika Afisi ya Kiranja wa Bunge la Kaunti.

Mpasuko baina yake na afisi hiyo ulishuhudiwa wakati Elachi na Bw Ngwele walikaripiana vikali nusura warushine masumbwi.

Bungeni Elachi alifokea madiwani, “Msinipigie kelele. Tutawapa muda mjitetee. Msiinue sauti dhidi yangu.”