Makala

BEATRICE MWAKIO: Nilivutiwa mno na maigizo ya 'Queen of the South '

February 16th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia, ndivyo wahenga walivyolonga. Tangu zama zile, msemo huo ungali na mashiko sio haba miongoni mwa wanajamii kwa jumla.

Akiwa mdogo alitamani kuhitimu kuwa daktari lakini hayo hayakutimia kutokana na kile anachosema kuwa pandashuka za kimaisha.

Hata hivyo ni mhudumu kwenye hospitali ya St Judes Medical Center, Komarock, Nairobi. Hayo tisa. Kumi, Beatrice Murunde Mwakio ni mwigizaji chipukizi anayepania makubwa miaka ijayo.

”Uigizaji kama taaluma nilianza kushiriki mwaka 2010 ingawa nilianza tangia nikisoma shule ya Msingi,” anasema na kuongeza kuwa anakumbuka vizuri akiwa mtoto alipenda sana kutazama kipindi cha Tausi kilichokuwa kinapeperushwa kupitia runinga ya KBC.

Kadhalika anasema alivutiwa zaidi kushiriki masuala ya maigizo baada ya kutazama kati ya filamu mahiri duniani iitwayo ‘Queen of the South’ ambayo ni miongoni mwa kazi zake Alice Braga mzawa wa Brazil.

”Katika mpango mzima natamani zaidi kuibuka staa katika uigizaji na kufikia viwango vya haiba kubwa duniani kama Mkenya, Lupita Nyong’o anayezidi kutesa katika filamu za Hollywood,” alisema na kuongeza kuwa pia anapania kukuza waigizaji chipukizi wanaume bila kuweka katika kaburi la sahau wanawake. Anadokeza kuwa anatamani zaidi kumiliki brandi yake hivi karibuni.

Dada huyu anajivunia kupata nafasi kushiriki filamu kadhaa ambazo zimepata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini.

Betty kama anavyofahamika kisanaa amebahatika kushiriki filamu kama ‘Njoro wa Uba’ (Maisha Magic) na ‘Majuto’ (K24) kati ya zinginezo.

Pia Murunde anayefanya kazi na kundi la Badilisha Arts anajivunia kufanya kazi na makundi tofauti ya kuzalisha filamu ikiwamo Zuia Theater na Pasha Media Production kati ya mengine.

Kwa filamu ambazo ameshiriki tangu mwaka 2010 anasema hadi leo huvutiwa na filamu iliyofahamika kama ‘Married in two weeks’ iliyotegenezwa na Pasha Media.

Ingawa jina lake halijapata mashiko katika filamu anasema kuwa angependa sana kufanya kazi na waigizaji mahiri hapa Afrika kama Mercy Johnson na Jackie Appiah. Wawili hao wanafahamika kwa kushiriki filamu kama ‘Dumebi the dirty girl,’ ‘Heart of a fighter,’ na ‘Beyonce’, ‘The Presidents daughter, ‘ mtawalia.

Ingawa anasema sekta ya uigizaji ina changamoto nyingi anashauri wenzie nyakati zote kuwa wavumilivu bila kutarajia utajiri wa haraka.

Pia anatoa mwito kwa maprodusa wakome kuwashushwa wanawake hadhi hasa kuwataka kimapenzi ili kuwapa ajira katika uigizaji.

”Katika mtazamo wangu itakuwa muhimu maprodusa kuwapa wasanii chipukizi nafasi ili kuonyesha talanta zao,” alisema na kuongeza waliowatangulia hawana budi kuwaonyesha wanaokuja mwongozo mwema katika tasnia ya maigizo. Kuhusu masuala ya familia alidinda kuyazungumzia huku akisema miaka ya sasa hakuna mteremko.