Bei ghali ya chakula cha mifugo yatishia kuzima jitihada za wafugaji

Bei ghali ya chakula cha mifugo yatishia kuzima jitihada za wafugaji

Na SAMMY WAWERU

JESSE Ngugi amekuwa katika sekta ya ufugaji kwa zaidi ya miaka minne.

Ni shughuli ya ufugaji-biashara aliyoingilia baada ya kuacha kazi ya udaktari.

Ngugi amesomea taaluma ya masuala ya kliniki.

Akiwa mfugaji wa ng’ombe wa kisasa na ambao wamemgharimu maelfu ya pesa kuwekeza, Dkt Ngugi analalamikia kuendelea kuongezeka kwa bei ya malisho ya mifugo.

“Ufugaji unafanikishwa kupitia chaguo bora la bridi na malisho yaliyoafikia ubora wa bidhaa na kuwa na virutubisho vya kutosha,” asisitiza.

“Hata hivyo, kuendelea kuongezeka kwa bei ya chakula cha mifugo kunatishia wafugaji wengi nchini.”

Ni hali ambayo imekuwa mbaya zaidi hasa baada ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19, ugonjwa ambao ni janga la kimataifa.

Ngugi na ambaye anaendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa eneo la Kaharate, Kaunti ya Murang’a, anasema mfuko wa kilo 70 umeongezeka kutoka Sh2,200 hadi zaidi ya Sh2,700.

“Ongezeko la Sh500 si mzaha, ilhali bei ya maziwa inasalia ilipokuwa,” alalamika mfugaji huyo.

Ana ng’ombe watano aina ya Friesian, na anasema awali alikuwa akijiundia lishe ila ongezeko la bei ya malighafi lilisitisha mpango huo.

“Kitambo ng’ombe alikuwa akizalisha kati ya lita 15 – 20 kupitia chakula cha kujitengenezea, kwa sasa kufikisha 10 ni kwa neema za Mungu.

“Upungufu huu unatokana na mahangaiko ya kutafuta malisho, kwa kununua nyasi maalum na mihindi,” afafanunua.

Anasema, manufaa ya kujitengenezea chakula cha mifugo humuwezesha kupata kilichoafikia ubora wa bidhaa kwa sababu hujumuisha madini na virutubisho muhimu kusaidia ng’ombe kuzalisha maziwa zaidi.

Mfugaji huyu, kwa sasa amekodisha ekari sita eneo la Murang’a ambapo hukuza nyasi aina ya mabingobingo (napier grass) na mahindi ili kuokoa ng’ombe wake.

“Nimekuwa nikiendea mihindi na pia mahindi Nakuru ili kuunda silage na hay, hatua ambayo ni ghali mno,” afichua.

Mahangaiko ya Dkt Ngugi si tofauti na ya Ruth Wanjiru, mfugaji eneo la Komothai, Kaunti ya Kiambu.

Ruth Wanjiru akilisha mbuzi wake wa maziwa, eneo la Kiambu na analalamikia ongezeko la bei ya chakula cha mifugo. PICHA | SAMMY WAWERU

Wanjiru hufuga kuku wa kisasa na wa kienyeji walioimarishwa na mbuzi wa maziwa.

Hufuga kuku kwa minajili ya biashara ya mayai, na wanapokomaa – ari kutaga inaposhuka huwageuza kuwa wa nyama.

“Chakula cha mifugo kimekuwa ghali mno, bei isipotathminiwa huenda siku za usoni maziwa na mayai yakawa adimu,” Wanjiru aonya.

Licha ya kuwa hujitengenezea malisho, Wanjiru pia hununua kile cha madukani.

“Chakula cha kuku hakinunuliki. Bei inazidi kupanda kila uchao,” Wanjiru ateta.

Esther Muthoni, mfugaji wa kuku wa kienyeji, mbuzi wa maziwa na ng’ombe Nyeri, naye anasema hana budi ila kutafuta njia mbadala kudumisha mradi wake kufuatia ongezeko la bei ya chakula cha mifugo nchini.

“Ng’ombe na mbuzi, huwasagia nyasi za mabingobingo na majani ya miti na maua ninayokuza kwenye ua,” Muthoni akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Aidha, ana mashine ya shughuli hiyo, inayotumia nguvu za umeme.

“Kuku, huwapa punje za mahindi,” Muthoni akakeza, akiihimiza serikali na wadauhusika kufanya hima kutathmini bei ya chakula cha mifugo, anayohisi ikiendelea kuongezeka wafugaji wengi hawatakuwa na chaguo ila kuuza wanyama wao.

Maduka ya kuuza malisho nayo hayajaepuka mjeledi wa ongezeko hilo, gharama wakiielekezea wateja.

“Watengenezaji wanasema bei ya malighafi inazidi kuongezeka. Wafugaji walioathirika ni wa kuku, wengi wakiishia kuasi kuwafuga,” aelezea David Njoroge, mmiliki na mhudumu wa duka la kuuza bidhaa za mifugo Ruiru Mjini.

Anafichua, kufikia sasa amepoteza zaidi ya asilimia 30 ya wateja wafugaji wa kuku.

Mahangaiko ya wafugaji tuliozungumza nao, yanaashiria hali na taswira ilivyo kwa mamia na maelfu ya wafugaji wenza nchini.

Huku serikali ikionekana kufumbia macho kilio cha wakulima na wafugaji, ushuru (VAT) wa juu unaotozwa bidhaa za kilimo, ufugaji na chakula umechangia mfumko huo kwa kiasi kikubwa.

Vilevile, ongezeko la bei ya mafuta ya petroli hususan mwaka huu ina mchango wake.

  • Tags

You can share this post!

Shirika la PrimRose laokoa walevi Gatundu Kaskazini

Echesa aondolewa lawama katika sakata ya Sh39Bn ya silaha...

T L