Habari

Bei ya dizeli na petroli yapanda, nayo ya mafuta taa yarudi chini

September 14th, 2019 1 min read

Na CAROLYNE AGOSA

BEI ya dizeli na petroli imeongezeka kwa Sh2.44 na Sh0.28 katika kila lita mtawalia baada ya kushuka Agosti.

Wenye magari jijini Nairobi watanunua lita moja ya dizeli kwa Sh103.04 na Sh112.81 kwa lita ya petroli.

Halmashauri ya Kudhibiti Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) imesema bei hizo mpya zitatumika kuanzia Septemba 15 hadi Oktoba 14, 2019.

Hata hivyo, bei ya mafuta taa nchini imeshuka na sasa itauzwa Sh100.64 kwa lita moja mjini Nairobi katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Bei hiyo imeshuka kwa Sh3.31 kutoka ile ya awali ya Sh103.95 kwa mujibu wa bei mpya zilizotolewa Jumamosi na Halmashauri ya Kudhibiti Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA).

Wakazi wa mji wa Mombasa, ambako shehena ya bidhaa za mafuta hutua bandarini kutoka soko la kimataifa, watanunua lita ya mafuta taa kwa Sh98.03.

Dizeli itanunuliwa Sh100.44 kwa lita moja huku petroli ikinunuliwa Sh110.19. Mjini Nakuru bei ya mafuta taa itakuwa Sh101.35 lita moja, ya dizeli Sh103.74 na petroli Sh113.30.

Mjini Eldoret mafuta taa yatauzwa Sh102.35 kwa lita, petroli itauzwa Sh114.29 nayo lita ya dizeli itanunuliwa kwa Sh104.74 ikilinganishwa na Sh102 mwezi Agosti.

Bei ya mafuta taa, dizeli na petroli katika Kaunti ya Kisumu – lita moja – itakuwa Sh102.35, Sh104.74 na Sh114.29 mtawalia.

Wakazi wa mji ulio mbali zaidi wa Isebania watalipia mafuta taa Sh104.29, petroli Sh116.22 na dizeli Sh106.68 kwa kila lita.