Habari Mseto

Bei ya kahawa nchini yaendelea kuimarika

April 12th, 2024 1 min read

Na KNA

KAHAWA ya Kenya imeendelea kuvutia bei katika Soko la Kahawa la Nairobi (NCE) kwa muda wa wiki mbili zilizopita.

Wakati wa mauzo ya kahawa wiki hii katika NCE, jumla ya magunia 26, 813 ya kahawa yalipata Sh1 bilioni ambayo yalipungua kidogo ikilinganishwa na Sh1.3 bilioni katika soko wiki jana.

Kiwanda cha Kahawa cha Karumandi katika Kaunti ya Kirinyaga kilichouza kahawa yake kupitia Alliance Berries Ltd kilipata bei nzuri huku kila gunia ya Gredi AA likiuzwa Sh50, 180.

Kiwanda hicho kilipata Sh6.6 milioni baada ya kuuza magunia 107 ya kahawa ya daraja la AA.

Viwanda vingine vilivyopata bei nzuri ya kahawa ni pamoja na kiwanda cha Kiunyu kikiwa na magunia 55 ya Gredi AA ambayo yalinunuliwa kwa Sh46, 410 kwa kila gunia huku viwanda vya Thangani na Nduma vilivyo chini ya New Kenya Planters Cooperative Union (KPCU) kila kimoja kikiuza magunia 112 ya ubora wa AA kwa kila kimoja kikipata Sh48, 230 kwa kila gunia moja.