Bei ya mafuta haitabadilika – Serikali

Bei ya mafuta haitabadilika – Serikali

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI kupitia kwa Tume ya Kusimamia Bei ya Kawi na Petroli (EPRA) Jumatano ilitangaza kuwa bei ya mafuta haitabadilika katika kipindi cha siku 30 zijazo.

Hii ina maana kuwa bei ya petroli aina ya Super itasalia Sh122.81 kwa lita moja jijini Nairobi na viunga vyake, dizeli itauzwa kwa Sh107.66 kwa lita huku mafuta taa ikiuzwa kwa Sh97.85.

Kulingana na EPRA bei hizo zinajumuisha ushuru wa VAT wa kima cha asilimia nane kulingana na mapendekezo ya Sheria ya Fedha ya 2018 na aina nyingine ya ushuru ambayo serikali hutoza bidhaa za mafuta.

Mnamo Machi 14, 2021 bei ya petroli iliongezeka kwa Sh7.63 kwa lita moja na kuibua malalamishi miongoni mwa Wakenya, haswa wenye magari.

Bei ya dizeli na mafuta taa pia zimepanda kwa Sh5.75 na Sh5.41 kwa lita moja.

EPRA ilisema kuwa ongezeko la bei ya mafuta mwezi huu umechangiwa na kupanda kwa bei ya bidha za petrol katika masoko ya kimataifa.

“Hii ni kwa sababu hitaji la mafuta linaendelea kupanda baada ya kushuka mwaka jana, kutokana na makali ya janga la Covid-19,” ikasema EPRA.

Kwa mfano, kulingana na asasi hiyo, bei ya petrol inayoagizwa kutoka nje ilipanda kwa asilimia 14.97 mwezi jana huku zile ya dizeli na mafuta taa zikipanda kwa asilimia 12.29 na 13.26, mtawalia.

Ongezeko hilo la bei ya mafuta ilichangia kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi, kama vyakula, na hivyo kuongeza mzigo mwa wananchi.

Ingawa bei ya mafuta kimataifa imekuwa ikipanda katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Kenya imelaumiwa kutokana na ushuru na ada nyingi zilizowekwa katika bei za mafuta.

Kwa mfano, kutokana na Sh122.81 ambayo ni bei ya petrol Nairobi kuanzia Machi 14, Sh57.33 zinawakilisha ushuru mbalimbali. Ushuru hizo zinajumuisha Sh5.40 ambao ni wa ustawi wa sekta ya petrol ambao ulipandishwa kutoka kiwango cha senti 40 mwishoni mwa mwaka jana.

Bei ya petrol inapofikisha katika bandari ya Kenya ni Sh49.84 kwa lita moja. Gharama ya uhifadhi na Sh3.25 kwa lita moja na ile ya usambazaji na faida ya kampuni za mafuta ni Sh12.39 kwa kila lita.

You can share this post!

Mbote asema wanafunzi walimpa changamoto

Mtambue msanii chipukizi anayetunga nyimbo kwa lugha sita...