Habari Mseto

Bei ya mafuta taa na dizeli yapungua, ya petroli yapanda

July 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

BEI ya mafuta taa itashuka kuanzia Jumatatu, kufuatia mwongozo mpya uliotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli nchini (EPRA).

Mamlaka hiyo Jumapili ilitangaza bei hizo mpya zitakazodumu kwa kipindi cha mwezi moja, kutokana na kupungua kwa gharama ya uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa hiyo kutoka mataifa ya nje.

Mbali na bei ya mafuta taa iliyoshuka kwa Sh2.31, dizeli pia ilishuka kwa Sh0.88 lakini mafuta ya Super yalipanda kwa Sh0.29.

Kupitia taarifa, Mkurugenzi wa EPRA Pavel Oimeke alisema bei mpya iliafikiwa baada ya kujumuisha asilimia nane ya ushuru wa ziada (VAT) ili kutimiza matakwa yaliyowekwa kwenye mswada wa kifedha wa 2018.

Jijini Nairobi, bei mpya ya kila lita ya petroli ni Sh 115.39, dizeli 103.88 na mafuta taa Sh109.97.

Jijini Mombasa lita ya petroli itauzwa kwa Sh112.74 huku dizeli na mafuta taa zikiuzwa kwa Sh101.25 na Sh99.35 mtawalia.

Mafuta taa jijini Kisumu yatauzwa kwa Sh103.67, dizeli Sh105.58 na petroli Sh116.85.Vile vile upungufu huo wa bei ya mafuta taa na dizeli utashuhudiwa mjini Nakuru ambako kila lita itauzwa Sh104.58 na Sh102.69 mtawalia huku ya petroli ikiongezeka na kuuzwa kwa Sh115.86.

Mjini Eldoret, Super Petrol itauzwa kwa Sh118.86, dizeli Sh105.59 na mafuta taa Sh103.68