Habari Mseto

Bei ya mafuta taa yapanda

August 14th, 2020 2 min read

NA MARY WANGARI

WAKENYA wanakabiliwa na hali ngumu bei ya bidhaa za mafuta ya taa ikitarajiwa kuongezeka kwa karibu mara sita zaidi, kufuatia tangazo lililotolewa Ijumaa na Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA).

Mabadiliko hayo yametokana na uaigizaji mpya wa bidhaa hiyo ambayo haijakuwa ikiingizwa nchini tangu Aprili.

Lita moja ya mafuta ya taa sasa itauzwa kwa Sh83.48 katika Kaunti ya Nairobi kuanzia hii leo (Jumamosi), kulingana na bei mpya zilizotangazwa jana EPRA.

Hii ina maana kuwa wateja watalazimika kulipia Sh18.03 zaidi ikilinganishwa na bei ya Sh65.45 kwa lita moja ya mafuta ya taa mwezi uliopita.

Kuongezeka huko kwa bei za mafuta ya taa ni pigo kuu kwa familia maskini huku idadi kubwa ya wananchi wakigeukia kutumia bidhaa hizo na kupunguza matumizi ya gesi ya kupikia, kulingana na utafiti uliofanywa na EPRA.

Hali hiyo imesababishwa na hatua ya uagizaji bidhaa hizo mnamo Julai wakati bei za mafuta ambayo hayajafishwa zilikuwa zimeimarika na kuuzwa Sh4,657 kwa kila pipa.

Hatua hiyo imesababisha kuongezeka kwa asilimia 28 katika bei ya bidhaa za mafuta ya taa zinazotegemewa pakubwa na jamii maskini kupata mwangaza vilevile, pamoja na viwanda vya kutengeneza rangi.

Aidha nyongeza hiyo ya Sh18.03 ni karibu mara sita zaidi ya kiwango kilichowekwa cha nyongeza ya Sh3.32 katika bei ya petroli aina ya Super hadi Sh103.80 kwa kila lita jijini Nairobi na nyongeza ya Sh2.57 kwa bei za bidhaa za dizeli.

Kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa za mafuta ya taa ambazo bei yake ilishuka hadi Sh62 kwa kila lita moja, kulijiri huku wauzaji bidhaa hizo wakikaa kwa muda wa miezi mitatu pasipo kuagizia bidhaa hiyo nchini hivyo kusababisha upungufu.

Data kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia katika kipindi cha wakati Kenya ilipoanza kutekeleza mikakati ya kudhibiti Covid-19, inaonyesha kuwa kiwango cha matumizi ya gesi kilishuka huku cha mafuta ya taa kikiongezeka.

Mikakati hiyo iliyoambatana na nyakati ngumu za kiuchumi, ilisukuma wananchi wengi kugeukia kawi nyinginezo za bei nafuu.

Data ya miezi sita tangu Januari 2020, inaashiria kuwa wateja walinunua tani 23,327 za gesi ya kupikia mnamo Juni ikilinganishwa na kiwango cha bidhaa hiyo cha tani 30,860 mnamo Mei.

Kushuka kwa matumizi ya gesi kwa asilimia 24 kulijiri wakati ambapo kiwango cha matumizi ya mafuta ya taa kilipanda maradufu mnamo Juni hadi kufikia lita 29.4milioni kutoka lita 15.4 milioni mnamo Mei.

“Katika kipindi cha Julai/Agosti, hakukuwa na bidhaa yoyote ya mafuta ya taa iliyopakuliwa katika Bandari ya Mombasa. Kutokana na hali hiyo, bei iliyopo ya mafuta ya taa imedumishwa lakini ikarekebishwa kuhusiana na ukusanyaji ushuru kwa kampuni za mafuta katika kipindi cha bei iliyotangulia,” ilisema EPRA katika ripoti kuhusu bei za mafuta mnamo Julai.