Bei ya mafuta yapanda tena

Bei ya mafuta yapanda tena

NA CHARLES WASONGA

GHARAMA ya maisha inatarajiwa kuendelea kupanda baada ya bei ya mafuta kupanda kwa kiwango cha Sh5.50 kwa lita moja kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Jumapili, Mei 15, 2022.

Hii ni baada ya Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) kutangaza nyongeza hiyo kupitia taarifa iliyotuma kwa vyombo vya habari Jumamosi jioni.

Bei ya aina zote za mafuta imeongezeka kwa Sh5.50 hivi kwamba petroli itauzwa kwa Sh150.12 kwa lita moja jijini Nairobi kutoka bei ya Sh144.62.

Dizeli itauzwa kwa Sh131 kwa lita kutoka Sh125.50 huku mafuta taa ikiuzwa kwa Sh118.94 jijini Nairobi kutoka Sh113.44.

Bei hiyo ambayo inaaza kutumika kuanzi Mei 14 hadi Juni 14, 2022 wakati bei mpya itatangazwa, ndio itakuwa ya juu zaidi katika historia ya taifa hili.

“Japo bei za mafuta aina za petroli, dizeli na mafuta taa zimepanda kwa kiwango cha Sh5.50 kwa lita moja, serikali itaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za mafuta ili kuwapunguzia mzigo raia. Serikali itaendelea kutumia pesa za Hazina ya Ustawi wa Sekta ya Petroli (PDL) kukinga wananchi kutokana na uwezekano wa bei kupanda zaidi,” EPRA ikasema katika taarifa hiyo.

Mnamo Mei 14, 2022 bei ya mafuta ilipanda kwa kiwango cha juu cha Sh9.90 na hivyo kufikisha bei ya petroli hadi Sh144.62 kwa lita moja jijini Nairobi na viunga vyake.

Bei ya dizeli ilifika Sh125.50 huku bei ya mafuta taa ikifika Sh113.44 kwa lita moja.

Bei hiyo ilipanda wakati taifa lilikuwa likikumbwa na uhaba mkali wa bidhaa hiyo, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini.

Hali hiyo ilipelekea kampuni chache za mafuta kuongeza bei ya mafuta zaidi ya bei iliyowekwa na serikali, na hivyo kupelekea Waziri wa Kawi Monica Juma kutisha kuziadhibu.

Duru zilisema kuwa uhaba huo wa mafuta ulisababishwa na hatua ya kampuni za mafuta kuhodhi bidhaa hiyo zikilalamikia hatua ya serikali kuchelewesha ulipaji wa Sh37 bilioni kama ruzuku kwa kampuni.

Lakini hata baada ya serikali kulipa pesa hizo kufuatia hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini bajeti ya ziada, uhaba huo wa mafuta uliendelea kushuhudiwa nchini.

Duru zilisema hali hiyo ilisababishwa na hatua ya kampuni za mafuta kuuza mafuta katika mataifa jirani ya Uganda na Tanzania ambapo bei ya bidhaa hiyo ni juu zaidi ikilinganishwa na Kenya.

Hii ni kwa sababu, serikali za mataifa hayo hayana sera ya kutoa ruzuku kwa kampuni za mafuta kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta.

Kwa mfano, nchini Tanzania lita moja ya mafuta inauzwa kwa Sh167.56 za Kenya kwa lita moja  ilhali nchini Uganda bidhaa hiyo inauzwa kwa Sh177 kwa lita.

  • Tags

You can share this post!

Malalamiko ya wabunge baada ya SRC kupunguza mapato yao

Haaland afunga bao katika mchuano wake wa mwisho kambini...

T L