Habari

Bei ya mafuta yapanda tena

July 14th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA watagharimika zaidi ndani ya kipindi cha siku 30 zijazo baada ya bei ya mafuta kupanda kufuatia tangazo lilitolewa na Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta Nchini (EPRA) Jumanne, Julai 14, 2020.

Bei mafuta ya petroli imepanda kwa Sh11.38 huku ile ya mafuta taa ikipanda kwa Sh2.98 nayo bei ya dizeli ikiongezeka kwa Sh17.30 kwa lita moja.

Hii ina maana kuwa wenye magari ya uchukuzi wa umma huenda wakapandisha nauli ikizingatiwa kuwa magari hayo mengi hutumia dizeli.

Katika kaunti ya Nairobi bei ya lita moja ya mafuta sasa itapanda hadi Sh100.48 kuanzia saa sita Julai 15 kutokana bei ya sasa ya Sh89.10

Nayo dizeli itapanda hadi Sh91.87 kwa lita moja kutoka Sh74.57 huku lita moja ya mafuta taa ikiuzwa kwa Sh65.45 kutoka Sh62.46

“Bei hizo zinajumuisha ongezeko la ushuru wa kwa jina Petroleum Development Levy unaotozwa petroli na dizeli na ushuru wa thamani ya ziada ya asilimia nane kulingana na Sheria ya Fedha ya 2018 na mabadiliko yaliyofanyiwa sheria mbalimbali za ushuru,” akasema Mkurugenzi wa EPRA Pavel Oimeke kwenye taarifa.

Ongezeko hilo la bei pia limechangiwa na bei ya petroli inayoagizwa kutoka ng’ambo ambayo ilipanda kwa kiasi cha asilimia 12.64 hadi dola 279.58 (Sh27,900) mnamo Juni.

“Nayo bei ya dizeli ilipanda kwa kiasi cha asilimia 232.16 hadi dola 302.15 (Sh31,200),” akasema Bw Oimeke.