Habari Mseto

Bei ya nyanya nchini haikamatiki

February 26th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WALAJI wa nyanya nchini hawana budi ila kufukua zaidi mfukoni kufuatia ongezeko la bei ya zao hili.

Mfumuko huu wa bei unatokana na kiangazi kinachoshuhudiwa kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita. Zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya hutumia kiungo hiki katika mapishi.

Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali, imebainika kwamba nyanya moja kubwa sasa inauzwa Sh10 katika masoko mbalimbali kaunti ya Nairobi, Machakos, Kiambu na Murang’a.

Kundi la nyanya tatu linagharimu Sh25, huku zile ndogo zikiuzwa nne Sh20.

Picha ya awali ya mkulima wa nyanya eneo la Mung’etho, Juja kaunti ya Kiambu, akizichagua tayari kuelekea sokoni. Picha/ Sammy Waweru

Hali si tofauti na maeneo ya Bonde la Ufa, Pwani, Magharibi mwa nchi, Nyanza na Mlima Kenya.

Awali, kabla ya Novemba 2018, moja kubwa ilikuwa ikigharimu Sh5, na baadhi ya masoko kundi la tatu Sh10.

“Nyanya hazipatikani, hazipo shambani kwa sababu ya kiangazi. Tunazopata ni kwa bei ghali,” alisema Mama Njambi, muuzaji wa bidhaa hii katika soko la Jubilee, Kiambu.

Licha ya zao hili kuadimika, Edwin Kabeti ambaye huuzia Zimmerman, Nairobi, alilalamikia kuhusu mawakala akisema wamechangia kupanda kwa bei.

Nyanya shambani. Picha/ Sammy Waweru

Alidai wanatumia nafasi ya kuwepo kwa ukame kukandamiza wafanyabiashara, na ili kuepuka hasara wanalazimika kuongeza bei.

“Wakati jua limeangaza, nyanya hazikosekani ikilinganishwa na msimu wa mvua kubwa. Kwa kiasi kikubwa mawakala wanachangia ongezeko la bei. Si wateja pekee wanaoumia, hata sisi wafanyabiashara,” aliteta Bw Kabeti.

Mawakala

Wakulima wengi kwa kuwa hawana soko la moja kwa moja la mazao, hulazimika kuuzia mawakala ili kuepuka kugharamika zaidi kando na gharama ya kulima, mbolea, dawa na wadudu. Derrick Mutugi, mkulima wa nyanya, vitunguu na pilipili mboga Ngoliba, Kiambu alisema nyanya zinazopatikana sasa ni za wanazaraa wanaotumia mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba. “Wenye vyanzo vya maji kama mito, vidimbwi na mabwawa ndio wanavuna,” alisema, akiongeza kuwa hutumia maji ya Mto Athi.

Serikali imekuwa ikihimiza wakulima kutumia mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kufanya kilimo. Sekta ya kilimo iligatuliwa mwaka wa 2013, kupitia katiba ya sasa iliyoidhinishwa 2010.