Bei ya omena kupanda wavuvi wakitii marufuku

Bei ya omena kupanda wavuvi wakitii marufuku

NA GEORGE ODIWUOR

HUENDA bei ya dagaa – omena – ikapanda kwa wiki chache zijazo baada ya wavuvi kutekeleza marufuku ya kuvua samaki wadogo katika Ziwa Victoria.

Wavuvi wengi kaika ziwa hilo wameacha kuvua omena kufuatia marufuku yanayolenga kuongeza idadi ya samaki.

Hata hivyo, baadhi wamepinga hatua hiyo wakisema hawawezi kuacha uvuvi kwa kuwa ndiyo njia ya kuwapa mapato.

Wanaopinga waliandamana katika ofisi za kamishna wa kaunti zilizoko kaunti ndogo ya Mbita mnamo Alhamisi wakisema hawatambui sheria inayopiga marufuku biashara ya omena.

Kwa wiki moja, wavuvi wamezuiwa kuvua omena katika ziwa hilo katika kile kinachotajwa kama hatua ya kulinda samaki wengine pia.

Wataanza kuwavua tena Januari 2023 samaki katika ziwa hilo watakapokuwa wameongezeka.

Marufuku hayo ni desturi ya kawaida ambayo ilinuiwa kuhakikisha kuwa idadi ya samaki wadogo inaongezeka. Kuongezeka kwa omena kunafaidi samaki wengine kwa kuwa wanawatumia kama chakula na kuwafanya wakue na kuongezeka pia.

Wavuvi walikuwa wakisitisha uvuvi kwa miezi minne kati ya Aprili 1 na Julai 31.

Hata hivyo, idadi ya watu ilipozidi kuongezeka na mahitaji ya samaki kuongezeka, wavuvi waliacha kusitisha shughuli zao wakihofia kupoteza mapato. Kulingana na Mkurugenzi wa uvuvi katika serikali ya kaunti ya Homa Bay, desturi hiyo ilitekelezwa mara ya mwisho kabla ya ugatuzi.

“Hatuna sheria inayosimamia kusitishwa kwa uvuvi kwa sasa. Ilani ilikuwa ikitumwa kutoka Idara ya Uvuvi kuagiza wavuvi wasiende ziwani, lakini chini ya ugatuzi, haiwezi kutekelezwa kwa sababu ya sheria tofauti katika kila kaunti,” alisema

“Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, shughuli za uvuvi zimeongezeka na kuathiri pakubwa ziwa hilo. Kwa wakati huu, Ziwa Victoria haliko jinsi lilivyokuwa mwongo mmoja uliopita,” akaongeza.

Kulingana na Bw Okoth, kaunti ya Homa Bay iliyo na ufukwe mkubwa wa ziwa hilo ilikuwa ikizalisha zaidi ya tani 50,000 za samaki kila mwaka kufikia 2010.

Kufikia 2017, uzalishaji ulipungua hadi chini ya tani 25,000 huku omena wakiathiriwa zaidi.

“Tunapoongea sasa, uzalishaji ni chini ya tani 10,000 na inatia hofu,” inasema afisi ya uvuvi. Marufuku hayo yalisukuma wavuvi kutafuta njia za kuokoa samaki wa aina fulani wasiangamie huku wakilinda chanzo chao cha mapato.

Majuzi maafisa wa usimamizi wa fuo walikutana na kuamua kusimamisha uvuvi wa omena ilivyokuwa desturi yao ili kurejesha ziwa hilo katika hali yake ya awali ya kuzalisha samaki kwa wingi.

Bw Okoth alisema kwamba maafisa kutoka wizara ya kilimo na uvuvi walihudhuria mkutano huo na kuunga pendekezo hilo ambalo walisema lina manufaa ya kiuchumi.

“Maafisa kutoka wizara waliona umuhimu wa kuweka marafuku hayo ili kuwezesha samaki kuongezeka. Ni usimamizi wa ufukwe unao jithibiti wenyewe na sio serikali inayowalazimisha kufanya hivyo,” alisema.

You can share this post!

Visa vya wizi wa mita za maji vyakithiri Malindi

Mpango maalumu wa Rais kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi...

T L