Habari Mseto

Bei ya unga wa mahindi yapanda

April 27th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WALAJI wa ugali hawana budi ila kuugharimia zaidi kufuatia mfumkobei wa bidhaa muhimu ambayo ni unga wa mahindi.

Ongezeko la bei ya bidhaa hiyo linashuhudiwa wakati ambapo taifa linapambana kudhibiti maambukizi ya Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Kwenye uchunguzi wa ‘Taifa Leo’, pakiti ya kilo mbili sasa inauzwa zaidi ya Sh150.

Kwa mfano, katika duka la jumla la Power Star, tawi la Zimmerman, Nairobi, unga wa Hostess pakiti ya kilo mbili inauzwa Sh159.

Hata ingawa kuna kipimo kinachogharimu Sh119, unga wa Mama ambao ni wa bei ya chini, ni ishara mwananchi wa kawaida ataendelea kuumia ikizingatiwa kuwa gharama ya maisha inaendelea kuongezeka.

“Tunakonunua pia tumeongezewa bei. Hatuna buda ila kugawana gharama hiyo na wateja,” mmoja wa wasimamizi wa Power Star, Zimmerman, na aliyeomba kubana jina lake ameeleza.

Bei ya bidhaa mbalimbali hususan za kula inaendelea kuongezeka kufuatia athari za corona nchini, virusi ambavyo vimesambaa kila kona ya ulimwengu.

Machi 2020 Rais Uhuru Kenyatta alihimiza wafanyabiashara kutoongeza bei ya bidhaa, haswa wakati huu taifa linapitia nyakati ngumu kwa sababu ya Covid–19.

Mfumuko wa bei ya unga wa mahindi unajiri licha ya malighafi kutengeneza mafuta ya petroli na dizeli kushuka kwa kiwango kikuu, kupungua au kuongezeko kwa bei ya mafuta, kukitajwa kama kigezo kinachoathiri bei ya bidhaa.

Mwaka 2018 aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alikuwa ameagiza pakiti ya kilo mbili unga wa mahindi nchini isiuzwe zaidi ya Sh75, wasagaji nafaka wakipinga vikali amri hiyo.

Tayari baadhi ya Wakenya wameanza kulalamikia njaa kutokana na hali ngumu ya maisha inayosababishwa na corona.

Wengi wamepoteza nafasi za kazi kufuatia biashara na baadhi ya kampuni na mashirika kufungwa.

Isitoshe, athari za Covid-19 zimeshinikiza baadhi ya kampuni kupunguza mishahara ya wafanyakazi, na kuwapa kadhaa likizo ya lazima.

Kimsingi, janga hili limeathiri kwa kiasi kikuu sekta ya biashara na uchumi.

“Nilifunga duka langu la saluni kwa hofu ya maambukizi ya corona. Kwa sasa sina njia nyingine kujipa kipato ambapo familia inanitegemea, unga nao ndio huo unaendelea kuwa ghali,” Dorine Kawira mkazi Nairobi amelalamika.

Ikizingatiwa kwamba ugali ni chakula kinachopendwa na Wakenya wengi, mfumkobei wa bidhaa hiyo utawaumiza.