Habari

Bei za bidhaa kupanda zaidi licha ya serikali kuahidi afueni

April 8th, 2020 2 min read

Na PAUL WAFULA

SERIKALI imependekeza kuongeza bei ya mkate, maziwa, gesi ya kupikia, dawa, petroli miongoni mwa bidhaa nyingine muhimu kwa mwananchi.

Bidhaa zingine ambazo zitaongezwa iwapo mswada wa marekebisho ya ushuru utapitishwa na Bunge ni neti za kuzuia kuuumwa na mbu na chanjo za kuzuia magonjwa hatari.

Katika hatua ambayo ni kinaya cha ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita kuwa atawakinga Wakenya kutokana na madhara ya virusi vya corona, serikali yake imependekeza marekebisho kwenye ushuru, ambayo badala ya kupunguza gharama ya maisha itaiongeza.

Wataalamu wametaja hatua hii kama kuwachezea Wakenya kwa kuwapunguzia baadhi ya kodi na kisha kutumia mbinu nyingine kuwaongezea gharama.

Kulingana na Rais wa Chama cha Mawakili (LSK) Nelson Havi kwenye barua kwa Karani wa Bunge la Taifa, hatua hizo zitakuwa na madhara makubwa kwa umma.

Kwenye mswada ambao umeandaliwa, gesi ya kupikia sasa itaanza kutozwa ushuru wa ziada (VAT) wa asilimia 14 na kusababisha kuongezeka kwa bei yake.

Serikali imekuwa ikihimiza Wakenya kutumia gesi kutokana na madhara ya mafuta taa na kuni kiafya na pia kulinda mazingira. Lakini sasa hatua ya kuongeza bei ya gesi inakiuka dhamira hiyo.

Bei ya mkate nayo itapanda kwani mswada huo unapendekeza kutozwa kwa VAT kwa mikate iliyookwa kwa unga aina nyingine isipokuwa ngano.

Hii ni kinyume na mipango ya kuhamasisha Wakenya kula aina nyingine za vyakula kama mikate iliyookwa kwa viazi vitamu na aina nyingine za unga, ambazo wataalamu wanasema ni bora kiafya kuliko unga wa ngano.

Pia imependekezwa kuongezwa kwa ushuru wa petroli, dizeli na mafuta taa, hali ambayo itaongeza bei ya bidhaa zingine za matumizi.

Kinaya kingine ni kuwa serikali inataka ushuru wa VAT wa asilimia 14 kwa dawa za kuua wadudu mashambani, wakati ambao wakulima wanakabiliwa na matatizo ya nzige na viwavi jeshi.

Serikali pia imeonekana kukosa umakini katika vita vya kumaliza plastiki baada ya kupendekeza ushuru wa asilimia 25 kwa kampuni zinazotengeza upya bidhaa za plastiki.

Hatua hii inafuta mafanikio ya kimazingira ambayo yametokana na kutumiwa kwa plastiki zilizotumika kutengeza bidhaa mpya.

Bei ya bidhaa pia itachangiwa kupanda na hatua ya kuondoa ridhaa ya umeme kwa viwanda.

Pendekezo lingine ambalo linaonyesha kutojitolea kwa serikali katika kukuza uchumi ni kuongezwa kwa ada za kuzuru mbuga za wanyamapori kwa kampuni za watalii.

Hii ni pigo kwa sekta ya utalii ambayo kwa sasa imeporomoka kutokana na janga la corona.