Akili Mali

Bei za vitunguu, sukumawiki na viazi zapanda mfumko ukiongezeka kwa asilimia 0.1

June 5th, 2024 1 min read

NA BENSON MATHEKA

BEI za bidhaa na huduma zilipanda katika mwezi wa Mei hadi asilimia 5.1 kutoka asilimia 5 mwezi Aprili, jambo lililochangiwa na kupanda kwa bei za vyakula na gharama ya uchukuzi.

Kulingana na Shirika la Taifa la Takwimu Kenya (KNBS) bei na kodi ya juu ya nyumba, umeme, gesi, na aina tofauti za mafuta pia zilichangia mfumuko wa bei Kenya mwezi uliopita.

Hii ilifanya bei ya kitunguu kuuzwa kwa Sh188.37 kwa kilo kutoka Sh177.02 huku kilo ya Spinachi ikiuzwa kwa Sh88.37 kutoka Sh74.78 mwezi wa Aprili.

Katika kipindi hicho, bei za sukumawiki ziliongezeka kwa asilimia 18.2, nyanya (asilimia 15) na viazi (asilimia 6.2).

Hata hivyo, bei za unga wa mahindi yaliyosagwa, unga wa mahindi ulioimarishwa, unga wa mahindi na unga mweupe wa ngano ilipungua kwa asilimia 3.2, 2.3, 1.6 na 1.3 mtawalia.

“Bei za nyumba, maji, umeme, gesi na aina zote za mafuta ziliongezeka kwa asilimia 1.2 kati ya Aprili 2024 na Mei 2024 kutokana na kupanda kwa bei ya kWh 200 na kWh 50 za umeme kwa asilimia 6.9 na asilimia 5.5 mtawalia. ” takwimu kutoka KNBS zinaonyesha.

Gharama ya usafiri iliongezeka kwa asilimia 0.2 baada ya bei ya petroli na dizeli kushuka kwa asilimia 0.5 na asilimia 0.7 mtawalia.

Hili ni ongezeko la kwanza la mfumuko wa bei wa kila mwezi Kenya, ambao umekuwa ukishuka tangu Januari mwaka huu, ukichochewa na kuimarika kwa mvua na utulivu wa shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu kuu za kimataifa kama vile dola ya Amerika.

Hata hivyo, hali hii inaweza kuwa ya muda mfupi baada ya mfululizo wa mafuriko kukumba nchi, na kusababisha uharibifu wa ekari ya mazao.

Kulingana na KNBS kwango cha sasa cha mfumuko wa bei kiko ndani ya kilichotarajiwa na serikali cha kati ya asilimia 2.5 na 7.5.