Michezo

Beijing Riders kuwakilisha Nairobi kwa fainali ya Chapa Dimba

March 22nd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KWA mara ya pili timu ya wasichana ya Beijing Raiders itawakilisha Mkoa wa Nairobi kwenye fainali za kitaifa za Mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three mwaka huu.

Kikosi hicho kitashiriki fainali za kitaifa kwa mara ya pili baada ya kushiriki fainali za kipute hicho cha Season One mjini Kakamega.

Beijing Raiders ilitwaa tiketi ya kushiriki kinyang’anyiro cha mwaka huu ilipoibuka malkia wa Mkoa wa Nairobi.

Beijing Raiders ya kocha, Mark Okwiri iliibuka malkia baada ya kuteremsha soka la kuvutia na kuchoma wapinzani wao bila huruma kwenye fainali zilizoandaliwa katika Shule ya Upili ya Jamhuri High, jijini Nairobi.

Timu ya Beijing Raiders ilipojishindia Sh200,000 majuzi. Picha/ John Kimwere

Beijing Raiders ilirarua waliokuwa mabingwa watetezi, Acakoro Ladies 6-0 katika fainali ya kusisimua. Salome Drailer aliifungia mara nne naye Facila Adhiambo alicheka na nyavu mara mbili.

Kwenye nusu fainali, vigoli hao walinyamazisha wenzao wa Kibagare Girls kwa mabao 3-0. Baada ya Beijing kutwaa ubingwa huo ilituzwa kitita cha Sh200,000.

Salome Drailer wa Beijing Raiders alizoa tuzo mbili: kama mfungaji bora wa kike kwa kutupia kambani magoli manne pia kuibuka mchezaji anayeimarika. Naye Esnas Kisia (Beijing Raiders) alituzwa kama mlinda bora kitengo cha wasichana katika fainali hizo.

”Bila shaka baada ya hali ya virusi hatari vya corona kutulia hatutaakuwa na lingine bali itatubidi tuanze maandalizi yetu kujiweka vizuri kushiriki fainali za kitaifa,” kocha huyo wa Beijing Raiders alisema na kuongeza kuwa wanafahamu bayana ngarambe ya mwaka huu haitakuwa rahisi.

Verine Achieng wa Beijing Raiders akirusha mpira. Picha/ John Kimwere

Katika mpango mzima anasema watajihadi kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wao kwenye kinyang’anyiro hicho.

Fainali za kipute hicho zimepangwa kuandaliwa mjini Mombasa mwezi Juni mwaka huu ingawa huenda mkurupuko wa virusi hatari vya corona ukachangia kusukumwa mbele. Mabingwa katika fainali za kitaifa (wavulana na wasichana) kila moja itatuzwa kitita cha Sh1 milioni.

Mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom yameibuka muhimu zaidi kwenye juhudi za kutambua na kukuza talanta za wachezaji chipukizi.

Kampuni ya Safaricom ambayo ndiyo wafadhili wakuu wa kipute hicho imetangaza kuwa imesitisha mashindano hayo kufuatia mkurupuko huo. Kabla ya kusitishwa kwa ngarambe hiyo michezo hiyo iliratibiwa kuelekea katika Mkoa wa Magharibi mwa Kenya.

Naomi Kibiringo (kulia) wa Kibagare Girls akwepa rafu ya mpinzani. Picha/ John Kimwere

Kufikia sasa jumla ya timu tano kitengo cha wasichana zimejikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa mwaka huu.

Timu hizo ni: Wiyeta Girls (Mkoa wa Bonde la Ufa), Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.