Michezo

Beki ajuta kutangaza biashara ya ngono ya 'mkewe' bila idhini

September 6th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

BEKI wa zamani wa West Ham United, Tomas Repka, anakodolea macho kusukumwa jela miezi sita kwa kutangaza huduma ya ngono inayotolewa na mke wake wa zamani Vlad’ka Erbova, kwenye mitandao ya kijamii bila idhini yake.

Repka, ambaye alikuwa West Ham miaka mitano kati ya mwaka 2001 na 2006, alihukumiwa katika mahakama ya Brno katika Jamhuri ya Czech.

Repka, 44, alipatikana na hatia ya kuchapisha matangazo matatu ya uongo ya huduma ya ngono mitandaoni akidai ni ya Erbova, ambaye walitalakiana mwaka 2016 baada ya kuwa bwana na bibi mwaka 2013.

Hata hivyo, beki huyu alikata rufaa kumaanisha kwamba jaji yuko huru kupunguza ama hata kuongeza hukumu hiyo ya kumsukuma Repka jela.

Mpenzi wa sasa wa Repka, mtangazaji wa vipindi kwenye runinga Katerina Kristelova, pia alijipata pabaya. Alitozwa faini ya Sh228,108 kwa kuhusika katika uhalifu huo.

Bi Erbova alisema, “Nilizirai nilipogundua aliyenitendea unyama huu. Sikuweza hata kulala. Nilihitaji ushauri kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya kiakili na ninapata matibabu.”

Repka aliomba msamaha. “Pole, nilikosa. Hata hivyo, uhusiano wangu na mke wangu wa zamani haukuwa mzuri. Sikuweza kuona mtoto wangu wa kiume, na hali ikawa mbaya kabisa.”