Kimataifa

Beki Harry Maguire aondolewa kwenye timu ya taifa ya Uingereza baada ya kuhukumiwa kifungo nchini Ugiriki

August 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA na beki wa Manchester United, Harry Maguire ametemwa na kocha Gareth Southgate kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza baada ya sogora huyo kupokezwa kifungo ambacho kimeahirishwa katika Kisiwa na Syros, Ugiriki.

Hadi maamuzi ya kesi iliyokuwa ikimkabili Maguire, 27, kutolewa mnamo Jumanne, nyota huyo alikuwa amejumuishwa na Southgate kwenye kikosi cha Uingereza ambacho kwa sasa kinajiandaa kwa kibarua kijacho cha kimataifa.

Beki huyo wa zamani wa Leicester City alipatikana na hatia ya kupigana, kukataa kutiwa nguvuni, kutumia umaarufu wake kukiuka sheria na kujaribu kuhonga maafisa wa polisi ili aachiliwe huru.

Southgate amesema kwamba kutemwa kwa Southgate kikosini mwake ni kwa minajili ya “maslahi ya pande zote husika”.

Kwa makosa aliyopatikana nayo katika eneo la Mykonos, Ugiriki. Maguire alipokezwa kifungo cha miezi 21 na siku 10 gerezani ila adhabu hiyo ikaahirishwa kwa miaka mitatu.

Hata hivyo, amewahakikishia mashabiki wake kwamba mawakili wake watakata rufaa.

“Naamini kwamba haki kuhusu suala hili zima itapatikana kwa sababu anayeathiriwa zaidi ni mimi, familia yangu na marafiki zangu,” akasema.

Akizungumza baada ya kufichua kikosi atakachokitegemea kwenye mechi zijazo za Uefa Nations League dhidi ya Iceland na Denmark mwezi ujao wa Septemba, Southgate alisema kwamba alikwisha wasiliana na Maguire na hana sababu zozote za kutilia shaka maelezo aliyompa.

“Maguire anasikitikia hali ambayo imechangiwa na tukio hilo ambalo kwa sasa limefanya dunia nzima kumwangazia kwa pamoja na timu ya taifa na waajiri wake Manchester United. Hakika, iwapo uchunguzi utafichua mengine na haya tunayoambiwa kwa sasa yabadilike, basi nitakuwa mwepesi wa kumrejesha kikosini,” akasema Southgate kwa kufichua kwamba tayari amezungumza na Man-United kuhusu maamuzi yake hayo.

Kati ya wanasoka ambao Southgate amewaita kambini mwa Uingereza kwa mara ya kwanza ni kiungo mvamizi wa Manchester City Phil Foden, fowadi Mason Greenwood wa Man-United na kiungo wa Leeds United, Kalvin Phillips.

Mshambuliaji Danny Ings wa Southampton na kipa Dean Henderson wa Man-United pia wamejumuishwa kikosini.

Ings ambaye amewajibishwa na Uingereza mara moja pekee hadi kufikia sasa, alipachika wavunia jumla ya mabao 22 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2019-20. Jamie Vardy wa Leicester aliyetawazwa mfungaji bora wa EPL alimshindia goli moja pekee.

Henderson ambaye hajawahi kuvalia jezi za timu ya taifa, aliwadakia Sheffield United kwa mkopo muhula huu na akawasaidia kukamilisha kampeni zao katika nafasi ya tisa katika msimu wao wa kwanza kwenye EPL.

Nahodha Harry Kane amejumuishwa kikosini licha ya fowadi huyo wa Tottenham Hotspur kulazimika kujitenga kwa siku baada ya kutua nchini Bahamas kwa likizo.

Kiungo Jack Grealish aliyewasaidia Aston Villa kuponea chupuchupu kushushwa ngazi kwenye EPL msimu huu, ameachwa nje ya kikosi cha Uingereza cha wanasoka 24.

Fowadi Raheem Sterling amejumuishwa kikosini kwa pamoja na mwenzake wa Man-City, Kyle Walker anayerejea baada ya muda mrefu.

Jordan Henderson na Alex Oxlade-Chamberlain wa Liverpool pamoja na Ben Chilwell na James Maddison wa Leicester wameachwa nje kwa sababu ya majeraha.

Uingereza wamepangwa kuvaana na Iceland mjini Reykjavik mnamo Septemba 5 kabla ya kuvaana na Denmark siku tatu baadaye jijini Copenhagen.