Michezo

Beki Ruth Ingosi wa Harambee Starlets ajiunga na AEL Champions nchini Cyprus

September 23rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Harambee Starlets, Ruth Ingosi ametia saini mkataba wa miaka miwili kambini mwa AEL Champions inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Cyprus.

Ingosi, 26, ameagana na Lakatamia FC ya Cyprus iliyomsajili kwa kandarasi ya miaka mitatu mnamo Januari 2020.

AEL walitua kileleni mwa jedwali la ligi nchini Cyprus katika msimu huu wa 2020-21 baada ya kuwacharaza Ethnikos Acha 13-0 mnamo Septemba 13, 2020. Hiyo mojawapo ya mechi tisa za raundi ya kwanza ambazo klabu hiyo imesakata hadi kufikia sasa msimu huu.

Kwa kujiunga na AEL, Ingosi anaungama na kipa wa Starlets, Annedy Kundu aliyeingia katika sajili rasmi ya klabu hiyo mnamo Septemba 15 kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuagana pia na Lakatamia.

Hadi alipokatiza uhusiano wake na Lakatamia, Kundu alikuwa amewajibishwa katika mechi 12 na akafungwa mabao 16. Kwa upande wake, Ingosi alikuwa amechezea Lakatamia michuano 12 na akawafungia mabao manne.

Kundu na Ingosi ni wanasoka wa zamani wa kikosi cha Eldoret Falcons kilichoambulia nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 26 katika Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake (KWPL) mnamo 2019.

Ligi ya Daraja la Kwanza la soka ya wanawake nchini Cyprus haijawahi kushuhudia tukio la vikosi kupanda wala kushuka ngazi tangu iasisiwe mnamo 2014 kwa kuwa ndiyo ya pekee nchini humo.

Hata hivyo, mabingwa wa ligi hiyo hupata nafasi ya kusakata kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ingosi na Kundu walianza kuwa andazi moto miongoni mwa klabu za bara Ulaya mnamo 2019 baada ya kutamba zaidi kambini mwa Starlets walionyakua ubingwa wa Cecafa Senior Challenge Cup kwa kuwatandika wenyeji Tanzania 2-0 jijini Dar es Salaam.

Kundu hakufungwa bao lolote katika kampeni nzima ya fainali hizo na akatawazwa Kipa Bora mwishowe.