Michezo

Beki wa Harambee Stars Musa Mohammed asajiliwa na Difaa El Jadida nchini Morocco

October 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Harambee Stars, Musa Mohammed, amejiunga rasmi na kikosi cha Difaa El Jadida kinachoshiriki Ligi Kuu ya Morocco.

Musa alisafiri kuelekea Morocco mnamo Oktoba 18 kabla ya kutia saini mkataba wa miaka mitatu aliopokezwa siku tatu baadaye.

Nyota huyo wa zamani wa FK Tirana nchini Albania anapata hifadhi kambini mwa Difaa baada ya kandarasi yake katika kikosi cha Nkana FC nchini Zambia kutamatika mnamo Julai 2020. Japo Nkana walikuwa radhi kurefusha mkataba wake katika Ligi Kuu ya Zambia (ZSL), nahodha huyo wa zamani wa Gor Mahia amesisitiza kwamba alipata ofa nzuri zaidi nchini Ethiopia.

“Ni fahari tele kuingia katika sajili rasmi ya kikosi cha haiba kubwa kufu ya Difaa El Jadida. Kubwa zaidi katika maazimio yangu kwa sasa ni kukabiliana na changamoto mpya katika kikosi cha waajiri wangu na kujiimarisha kitaaluma,” akasema Musa.

Musa, 29, alijiunga na Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi na washindi mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2010 baada ya kuagana na FISA Academy jijini Nairobi. Akiwa Gor Mahia, Musa ambaye ni nduguye mdogo mwanamasumbwi Fatuma Zarika, alinyanyua mataji manne ya Ligi Kuu, Kombe la Top 8 Super Cup, ubingwa wa Charity Cup na ufalme wa SportPesa Super Cup.

Aliagana na Gor Mahia kwa kipindi kifupi mnamo 2017 na kutua Albania kuvalia jezi za FK Tirana waliomwajibisha mara nne pekee kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Nkana FC mnamo 2018. Aliongoza Nkana kutwaa mataji ya ABSA Cup, Charity Cup na Ligi Kuu ya ZSL mnamo 2019-20.

Kwa kutua Morocco, Musa anaungana na wanasoka wazawa wa Tanzania – Simon Msuva na Nickson Kibabage katika kikosi hicho kilichokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro League) katika nafasi ya 11 kwa alama 35 kutokana na mechi 30 za msimu wa 2019-20.

Kikosi cha Difaa El Jadida kina kiu ya kusajili matokeo bora zaidi chini ya mkufunzi mpya Abdel-Haq Bashikha aliyeaminiwa kumrithi Anas Ahla mwishoni mwa muhula uliopita.