Michezo

Beki wa Stars kuhamia Angola

July 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Harambee Stars, Johnstone Omurwa amethibitisha kwamba yuko pua na mdomo kukatiza uhusiano wake na Wazito FC na kuingia katika sajili rasmi ya Petro Atletico nchini Angola.

Maamuzi ya Omurwa ya kukubali ofa ya mabingwa hao mara 15 wa Ligi Kuu ya Angola ni zao la kushauriwa pakubwa na washikadau mbalimbali, akiwemo fowadi wa zamani wa Gor Mahia, Jacques Tuyisenge ambaye kwa sasa ni mchezaji wa kikosi hicho.

Nyota wa sasa wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga ndiye Mkenya wa kwanza kuwahi kuchezea Atletico alipojiunga na miamba hao wa soka jijini Luanda mnamo 2007.

“Vinara wa Atletico walinijia mwishoni mwa mwezi uliopita wakiwa na ofa ya Sh10 milioni ili kuwashawishi Wazito FC kuniachilia. Wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kurasimisha uhamisho wangu.”

Nyota ya Omurwa ilianza kung’aa zaidi tangu kocha Francis Kimanzi apokezwe upya mikoba ya Harambee Stars mnamo Agosti 2019. Chini ya kocha huyo wa zamani wa Tusker na Mathare United, Omurwa amekuwa akiwajibishwa mara kwa mara katika mechi za timu ya taifa.

Wakati uo huo, Dennis Gicheru ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito FC, amethibitisha kwamba kikosi hicho kimeagana rasmi na masogora wawili zaidi siku chache baada ya kufurusha jumla ya wachezaji 12.

Kiungo Lloyd Wahome na mshambuliaji Paul Kiongera ndio wanasoka wa hivi karibuni zaidi kubanduka kambini mwa Wazito.

Wahome alijiunga na Wazito mnamo mnamo Machi 2019 baada ya kuvunja ndoa yake ya miaka mitano na mabingwa mara 11 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Tusker FC. Kiongera ambaye pia amewahi kuvalia jezi za wanabenki wa KCB na Simba SC nchini Tanzania, alisajiliwa na Wazito kwa mkataba mfupi mnamo Januari 2020.

Paul Acquah (Ghana), Issifou Bourahana (Togo), Augustine Out (Liberia) na Piscas Kirenge (DR Congo) ni wanasoka raia wa kigeni ambao walikuwa miongoni mwa 12 waliotimuliwa na Wazito FC mnamo Alhamisi iliyopita.

Wachezaji wa humu nchini ambao pia wamebanduliwa kutoka kikosi cha Wazito ni aliyekuwa fowadi wa SoNy Sugar Derrick Otanga, kipa mzoefu Steven Njung’e, kiungo Teddy Osok, mshambuliaji wa zamani wa Tusker Victor Ndinya na kipa chaguo la kwanza katika kampeni za msimu jana, Kevin Omondi aliyewahi pia kuvalia jezi za SoNy Sugar.

Kikosi cha Wazito kwa sasa kinamezea mate wanasoka Benson Omalla, Fidel Origa na Maurice OJwang kutoka Western Stima. Watatu hao wako pia kwenye rada ya Nairobi City Stars.