Makala

BELINDA ODHIAMBO: Usikubali kuvunjwa moyo na visiki katika uigizaji

November 10th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NDIO ameanza kujituma katika masuala ya maigizo na anasema analenga kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha anafikia viwango vya kimataifa miaka ijayo.

Ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaoibukia wanaopania kuvumisha tasnia ya filamu hapa nchini.

Martha Belinda Odhiambo aliyeanza kujituma katika masuala ya maigizo mwaka 2017 ni mwigizaji na mwana mtindo chipukizi hapa nchini.

”Kwangu nashiriki uigizaji kama ajira kwa kuzingatia tumeshuhudia wengi wamejijenga kimaisha kutokana na burudani ya maigizo,” anasema na kuongeza kuwa alitamani kuwa mwana maigizo tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya Msingi.

Kadhalika kisura huyu anasema analenga kukuza kipaji chake akomae hadi kushiriki filamu za Hollywood.

Katika mpango mzima anasema anataka kufikia kiwango chake Ophra Winfrey mzawa wa Marekani ambaye ni kati ya maprodyuza wa vipindi vya televisheni pia waigizaji mahiri duniani. Anasema msanii huyo amemtia motisha zaidi katika uigizaji.

Kadhalika anasema alichochewa zaidi kushiriki uigizaji miaka ya 2008 na 2009 alipotazama filamu kadhaa za hollywood ikiwamo ‘High School Musical’ na hapa nchini ‘Waridi’ hasa jinsi Barbara Chepkoech alivyoigiza kwenye filamu hiyo.

Kadhalika anadokeza kuwa angependa kufanya kazi na waigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Ncheta Rachael Okwonko aliyeigiza filamu ya ‘Left over’ na ‘Zee World Madness’ kati ya zinginezo.

Pia Vernee Watson-Johnson mzawa wa Marekani aliyeshiriki filamu ya ‘Mandela Effect’. Hapa nchini anatamani kushirikiana nao Catherine Kamau na Nice Githinji kati ya wengineo.

Demu huyu ni miongoni mwa wasanii wanaofanya kazi chini ya brandi mpya iitwayo Badilisha Art Production wanakoendelea kuzalisha filamu iitwayo ‘Stuck in the Middle.’

Anajivunia kushiriki filamu maarufu inayofahamika kama ‘Barshita’ ambayo ilipata mpenyo kupeperushwa kupitia Maisha Magic East. Pia ‘Breaking Egg’ iliyozalishwa na BMP Enternaiment ambayo huonyeshwa kupitia YouTube.

Kando na kundi hilo pia amefanya kazi ya uigizaji na makundi mengine ikiwamo: Future Art Production, The Theater Company na BMP Enternaiment. Picha/ John Kimwere

Kuhusu changamoto anasema amekumbana na visa vya kufanya kazi na kutolipwa jambo ambalo huvunja wengi wao moyo. ”Pia jamii ina dhana fulani kuwa waigizaji ama wasanii kwa jumla hawana nidhamu hali ambayo huchangia wengi wetu hasa wanawake kutoheshimiwa,” alisema.

Ndiyo ameanza kupiga ngoma lakini siyo mchoyo wa mawaida maana anasema amejifunza mengi. Anawashauri waigizaji wanaokuja kwenye gemu wajifunze kuhudhuria majaribio na kutengeneza uhusiano mwema na wadau ili kusaidiana wakati nafasi zinapotokea.

Kadhalika anawaambia wanapojitosa katika uigizaji kamwe wasijiwekee matamanio ya kupata umaarufu haraka maana tasnia ya filamu imejaa changamoto chungu mzima.

Kwa jumla anatoa mwito kwa wasanii chipukizi kutovunjika moyo kutokana na changamoto wanazopitia.

”Jambo lingine ni muhimu kwa wanaohisi wana talanta ya uigizaji, muziki au taalamu yoyote wanastahili kujizatiti pia kujiamini wanaweza bila kusikiza wanavyopondwa na wasiopenda wenzao wakipiga hatua kimaendeleo,” alisema.

Vile vile anasema ili sanaa ya maigizo ipige hatua hapa nchini itabidi serikali iweke miundo msingi bora kusudi itambulike. Aidha anadokeza kuwa serikali inastahili kuondoa vikwazo zingine ili wahusika kuwa uhuru kufanya shughuli zao bila vizuizi.