Michezo

Ben Foster kupangulia Watford mashuti hadi afikishe miaka 39

June 12th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Ben Foster ametia saini mkataba mpya wa miaka miwili ambao kwa sasa utamdumisha kambini mwa Watford hadi atakapofikia umri wa miaka 39.

Mlinda-lango huyo alivalia jezi za Watford kwa mara ya kwanza mnamo 2005 akihudumia kikosi hicho kwa mkopo kutoka Manchester United. Tangu wakati huo, amechezeshwa mara 150 katika kipindi cha misimu miwili.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza amewajibishwa katika mechi zote za hadi kufikia sasa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na akapangua jumla ya makombora 89.

Anatazamiwa kuwa mwokozi wa Watford ambao kwa sasa wananing’inia pembamba mkiani mwa jedwali kwa pamoja na Bournemouth, Aston Villa na Norwich City.

Kikosi hicho kitarejelea kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Leicester City mnamo Juni 20 chini ya kocha Nigel Pearson.

Sogora mwingine ambaye amerefusha muda wa kuhudumu kwake katika soka ya EPL ni mvamizi wa Liverpool, Adam Lallana ambaye kwa sasa atasalia uwanjani Anfield hadi mwishoni mwa msimu huu.

Nyota huyo mzawa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 32, alitarajiwa kuagana na Liverpool baada ya kandarasi yake kutamatika mnamo Juni 30, 2020.

Liverpool ambao kwa sasa wanajivunia pengo la alama 25 kileleni mwa jedwali la EPL wanatazamiwa kutia kapuni ubingwa wa kipute hicho msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Wamepangiwa kuvaana na Everton katika gozi la Merseyside mnamo Juni 21 uwanjani Goodison Park. Liverpool watafunga rasmi kampeni za EPL muhula huu dhidi ya Newcastle United mnamo Julai 26 ugani St James’ Park.

Mbali na Lallana, mwanasoka mwingine wa Liverpool ambaye amerefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Anfield ni kipa Andy Lonergan, 36, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kuwa kizibo cha Lisson Becker aliyekuwa akiuguza jeraha.

Wepesi wa Lallana kupata majeraha mabaya umemvurugia misimu yake kambini mwa Liverpool ambao amewachezea jumla ya mechi 15 na kufunga bao moja hadi sasa msimu huu.

Aliingia katika sajili rasmi ya Liverpool mnamo 2014 baada ya kushawishiwa kuagana na Southampton kwa kima cha Sh3.5 bilioni. Usajili wake ulifanikishwa na kocha Brendan Rodgers ambaye kwa sasa anayahemea maarifa yake kambini mwa Leicester.