Makala

SANAA: Bendi ya Ricky na Marafiki ina wanachama wenye tajriba

February 5th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

ILIANZISHWA mwaka 2010 baada ya Ricky Nanjero kuja pamoja na marafiki zake kuunda bendi ambayo walikiita Ricky na Marafiki.

Walitumia vifaa vinne – ala za muziki – ambazo ni ngoma, saxophone, kinanda aina ya bass keyboard kabla ya kuongeza ala ya marimba ‘percussion’.

Baada ya kuongeza ala hiyo walirekodi albamu nne kwa majina Tucheze (2011), So Simple (2013), Soul Food (2016) na Soko Huru za mwaka 2018 hadi 2019.

Mnamo mwaka 2018, aliungana na wasanii ambao ni pamoja na Papi Odeq, John Were, Edward Baraza na Michael Okinyo ambao walipata umaarufu kupitia albamu ya Soko Huru.

Jina hilo ‘Soko Huru’ lilikuwa na maana ya kuwawezesha kuuza muziki wao katika nchi zingine barani Afrika na ulimwenguni kote bila vizuizi.

“Muziki wetu unazungumzia mambo ambayo hufanyika kila siku katika maisha ya binadanu,” akasema Nanjero.

Ili kuufanikisha mradi huo, kila mwanachama wa bendi hiyo alikuwa na ujuzi wa kipekee ambao aliutumia katika bendi hiyo.

Katika bendi hiyo, Nanjero alileta ujuzi wake katika muziki wa Afro-Jazz, uandishi na upangaji wa nyimbo.

Odeq naye aliuleta ujuzi wake katika ala ya marimba.

Pia ana ujuzi katika uandishi wa nyimbo na filamu.

Were ana ujuzi katika gita baada ya kucheza ala hiyo tangu utotoni.

Wengine ni pamoja na Dkt Michael Okinyo ambaye anacheza piano.

Vilevile Okinyo ni mjuzi katika taaluma ya masula ya afya (medical officer).

Edward Solomon Baraza ana ujuzi wa kucheza ngoma.

“Naamini muziki wetu ni wa kipekee kwani tunaitumia lugha ambayo ni rahisi kuelewa na mambo tunayoyazungumzia yanaathiri kila binadamu,” aliongeza Nanjero.