Habari Mseto

Benki Kuu yadinda kupandisha kiwango cha riba

May 28th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wakenya wamepata afueni baada ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) kukataa kupandisha kiwango cha mwisho cha riba kwa benki za humu nchini.

CBK ilitangaza kuwa bado kiwango hicho ni asilimia tisa, kwa mara ya sita mfulululizo wakati ambapo benki zinaendelea kunyima sekta ya kibinafsi mikopo.

Kulingana na kamati ya sera ya kifedha, kiwango hicho hakikupandishwa ili kudhibiti mfumko wa bei ya bidhaa na kudumisha uwezo wa shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni.

Katika taarifa, CBK ilisema ukopeshaji kwa sekta ya kibinafsi umekua kwa asilimia 4.9 katika muda wa miezi 12 kufikia Aprili, ikilinganishwa na asilimia 4.3 Machi.

Benki hiyo ilisema kiwango cha ukopeshaji kwa sekta ya kibinafsi kinatarajiwa kuimarika zaidi mwaka huu, licha ya pingamizi za sekta hiyo.

Hata hivyo, ukopeshaji haujafikia kiwango kilichotarajiwa na CBK cha kati ya asilimia 12 na 15, kinachoweza kuhimili ukuaji wa uchumi.

“Kamati hiyo ilisema kuwa matarajio kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa bado yanaweza kuafikiwa, lakini kuna haja kubwa ya kuwa makini kuhusiana na athari za ongezeko la bei ya chakula na mafuta,” alisema gavana wa CBK Patrick Njoroge, baada ya mkutano wa kamati hiyo Jumatatu.

Kulingana na CBK, ukopeshaji kwa sekta ya kibinafsi unatarajiwa kuimarika mwakani kutokana na kuzinduliwa kwa apu ya ukopeshaji kwa biashara ndogo na za wastani.