Habari Mseto

Benki mashakani kuhusu uuzaji wa nyumba

August 8th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA ameishtaki benki kwa kuuza jumba lake kwa bei ya chini na kuomba mahakama kuu iamuru alipwe fidia ya Sh34 milioni.

Bi Mary Wanjiru Chege pamoja na kampuni yake ijulikanayo Nakuru Machinery Services Limited ameishtaki benki ya Ecobank kwa kuuza nyumba yake yenye thamani ya Sh34milioni kwa bei ya Sh15 milioni.

Mbali na fidia hiyo, Bi Chege anaomba mahakama kuu iamuru benki hiyo imrudishie Sh34 milioni na pia kumlipa gharama ya Sh20 milioni.

Mlalamishi huyu kupitia kwa wakili Titus Koceyo amesimulia kuwa mnamo 2015 alikopa pesa kutoka kwa benki ya Ecobank kufadhili mradi wa unyunyiziaji maji shamba wa Navemit Irrigation Scheme Phase I katika kaunti ya Turkana.

Kabla ya kupewa mkopo huo benki ya Ecobank ilifanya utafiti kuhusu thamani ya jumba la Bi Chege alilotumia kama dhamana na kupata thamani yake kuwa Sh30 milioni mnamo 2015.

Utafiti ulifanywa na kampuni ya Acumen Valuers mnamo Aprili 21, 2015.

Kampuni hiyo ilisema kuwa endapo jumba hilo lingeuzwa kwa bei ya chini ingeliuzwa kwa bei ya Sh22.5 milioni.

Lakini mlalamishi alisema baada ya utafiti kufanywa mikakati iliwekwa apewe mkopo huo ndipo wakaafikiana kuwa atakuwa analipa mkopo huo kwa asili mia 21.

Baada yam waka mmoja , Bi Chege anasema kuwa benki hiyo ilimpelekea arifa alipe mkopo aliokuwa anadaiwa katika muda wa siku 45.

“Kabla ya muda huo kumalizika benki hiyo ilitangaza itauza kwa njia ya mnada jumba lake,” anasema Bi Chege.

Kabla ya kuuzwa kwa dhamana aliyotoa kuthamini mkopo huo , Bi Chege anasema kuwa benki hiyo ilipasa kumpa muda wa kulipa deni hilo.

Amesema benki hiyo iliuza moja kwa moja makazi yake kinyume cha sheria.

“Uuzaji wa benki hiyo haukufanyika mahala ilipotangaza kwa vile nilienda pale na sikushuhudia uuzaji ukiendelea,” anasema mlalamishi.

Mbali na hayo mlalamishi anasema kuwa benki hiyo ilimruhusu mtu kutoka makao yake makuu kununua makazi yake kwa bei ya Sh Sh15,450,000.

Mnunuzi huyo alilipa Sh Sh3,862,500 badala ya kiwango cha pesa kinachokubalika kisheria.Pesa hizo alizilipa baada ya siku mbili kisha akalipa Sh4milioni nyingine.

Kwa muda wa siku 90 mnunuzi huyo alikuwa hajakamilisha kulipa pesa hizo.

“Udadizi niliofanya ulibaini kwa benki hiyo iliuza makazi yangu kwa pupa ndipo ininyime fursa ya kuinunua,” alisema mlalamishi.

Mahakama ilielezwa benki hiyo ilikuwa inalipwa mkopo huo na bodi ya kitaifa ya unyunyiziaji maji (NIB) kupitia kwa akaunti yake.

Mlalamishi amewasilisha mahakamani ushahidi jinsi mkopo huo ulikuwa unalipwa na kwamba “kufikia sasa hajapewa nakala za akaunti yake na benki hiyo kuonyesha kiwango alichokuwa analipwa.

“Jumba langu lililiuzwa kwa njia ya ufisadi na benki hiyo. Naomba uuzaji huo ufutiliwe mbali,” anaomba Bw Koceyo anayeongeza , “sheria za benki zilikiukwa kabla ya kuuzwa kwa thamana hiyo.”

Bi Chege anaomba mahakama kuu ifutilie mbali kuuzwa kwa shamba lake na kuamuru benki hiyo imlipe fidia