Habari Mseto

Benki ya Diamond yavuna faida ya Sh11 bilioni

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

BENKI ya Diamond Trust imetangaza ongezeko la asilimia tisa la faida kabla ya kutozwa ushuru.

Katika mwaka uliokamilika Desemba 31, 2018, benki hiyo ilipata faida ya Sh11 bilioni, na kuvunja rekodi.

Kulingana na benki hiyo, faida hiyo ilitokana na kuimarika kwa operesheni zake, ubunifu na kuhifadhi wateja.

Mali ya benki hiyo ilikua hadi Shs 378 bilioni, ongezeko la asilimia nne zaidi ya kiwango cha mwaka uliotangulia kwa kuongozwa hasa na kiwango kikubwa cha fedha zilizohifadhiwa humo na wateja wake hadi Sh 283 bilioni, kilichoongezeka kwa asilimia sita ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Nasim Devji, Meneja Mkurugenzi wa DTB na Afisa Mkuu Mkurugenzi alisema, “Tunafurahia sana kwamba DTB ilipata faida kubwa. Hii ni ithibati kuwa benki inaweza kukabiliana na changamoto, na uvumilivu wa wateja wake Afrika Mashariki.”

Matawi ya DTB Tanzania, Uganda na Burundi yalichangia asilimia 25 ya mali ya kampuni na faida ya asilimia 16.

“Matokeo hayo yalitokana na nafasi dhabiti ya kampuni sokoni na historia yake Afrika Mashariki katika kuhudumia wateja wake. Pia, msingi bora wa washikadau huongeza nguvu yet,” alisema Bi Devji.

Kulingana na taarifa, mikopo ya wateja ilipungua kutoka Sh13 bilioni hadi Sh12.1 bilioni.

Kutokana na hilo DTB, imependekezo mgao wa kwanza na wa mwisho wa Sh2.60 kwa kila hisa kama mwaka uliotangulia licha ya kuwa mapato kwa kila hisa yaliongezeka kidogo kutoka Sh23.73 hadi Sh 23.91.