Habari

Benki ya Dunia yaipa Kenya mkopo wa Sh75b, deni sasa lakaribia Sh6 trilioni

May 29th, 2019 2 min read

PAUL WAFULA na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Benki ya Dunia (WB) imeipa Kenya mkopo wa Sh75 bilioni na kuongezea wananchi mzigo wa madeni kutoka mataifa ya kigeni.

Benki hiyo iliidhinisha mkono huo Jumatano ambao ulisema utafadhili mageuzi katika sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kuimarisha uzalishaji na mapato yao.

“Mageuzi ambayo yatafadhiliwa kwa mkopo huu yanajumuisha kupunguzwa kwa bei ya pembejeo za kilimo ambazo zitafikiwa na wakulima, kupunguza ufisadi katika ununuzi na usambazaji wa mbolea, kuweka mikakati ya kuwezesha wakulima kupata mkopo kwa urahisi na kupunguza hasara inayotokea baada ya mavuno,” Benki ya Dunia katikla taarifa.

Benki hiyo pia ilisema mkopo huo utasaidia kufadhili sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili Wakenya waweze kupata huduma za intanet kando na kufadhili utengenezaji wa kitambulisho cha kidijitali.

“Kimsingi, mkopo huo utaimarisha uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi wake kwa kupunguza mtagusano katika maafisa wa serikali na wananchi, hali ambayo itapunguza ufisadi,” taarifa hiyo ikaongeza.

Hazina ya Kitaifa iliiandikia WB mnamo Machi mwaka huu ikiombo mkopo wa kuisaidia kufadhili bajeti yake.

Kwa kuwasilisha ombi hilo, serikali ilikwenda kinyume na mwenendo wake wa miaka kumi ambapo iliepukana na mkopo taasisi hiyo ya kimataifa kwa ajili ya kupiga jeki bajeti yake.

Chini ya utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, Kenya alichelea mkopo wa aina hii ambapo misaada kutoka kwa Benki ya Dunia ilikuja kwa njia ya ufadhili wa miradi.

Wachanganuzi wa masuala ya fedha na uchumi wameonya kwamba Kenya inakopa kupita kiasi. Wanasema hii inaonyesha kuwa Kenya inakabiliwa na changamoto ya kifedha hali inayodhihirika kupitia kupungua kwa mapato na kushindwa kwake kulipa madeni yake.

Hivi majuzi, Taasisi ya Maswala ya Uchumi (IEA) ilionya kuwa Kenya inakabiliwaa na hatari ya kushindwa kulipa madeni yake miaka 10 baada ya sasa ikiwa uchu wake wa kukopa hautapunguzwa.

Kufikia Septemba 2018, kiwango cha madeni ya Kenya kilikuwa kimefikia Sh5.1 trilioni, na mkopo wa hivi majuzi huo ukapandisha deni hili hadi Sh5.5 trilioni kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Lakini hazina ya kitaifa imetetea mikopo hiyo na kupinga madai kuwa Kenya imefilisika.

Waziri wa Fedha Henry Rotich alisema kuwa Sh75 bilioni ambapo Kenya ilipokea kutoka kwa Benki ya Dunia itasaidia kufadhili miradi ya serikali yaliyoko chini ya Agenda Nne Kuu.

“Huu mkopo wa Benki ya Dunia unalenga kupiga jeki maendeleo. Unapeanwa katika mataifa mengi. Ndio ni wa kusiadia katika ufadhili wa bajeti lakini haiwezi kuongeza mzigo wa madeni,” Bw Rotich akasema bila kufafanua zaidi.

Mkopo huu unajiri wiki mmoja baada ya Kenya kupata mkopo wa Eurobond wa kima cha Sh210 bilioni. Bw Rotich alisema pesa hizo zitatumiwa kulipia baadhi ya madeni ya serikali ambayo muda wao wa kulipwa utaanza Julai mwaka huu.

Hii ni kama vile Sh342 bilioni ilizokopa kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi Mombasa.

Ni mapema mwaka huu Serikali ya China iliikataa kuipa Kenya mkopo mwingine wa Sh380 bilioni wa kufadhili ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu ikisema “hatujapata hakikisho kuhusu faida ya mradi huo.”