Habari Mseto

Benki ya Equity yapata mwenyekiti mpya

August 28th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

BENKI ya Equity imemteua balozi Erastus Mwencha awe mwenyekiti mpya wa bodi yake.

Bw Mwencha alichukua jana Alhamisi wadhifa huo kutoka kwa Prof Isaac Macharia ambaye alipandishwa cheo na kuteuliwa mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Equity Holdings.

Akizungumza baada ya kupokezwa wadhifa huo, Bw Mwencha aliahidi kukuza benki hiyo kiuchumi na pia kuboresha mazingira yake kibiashara na jinsi inavyowahudumia wateja wake.

“Nachukua kazi hii wakati ambapo athari za virusi vya corona zimelemaza sekta mbalimbali za uchumi. Nitahakikisha benki hii inaendelea kupanua matawi yake na kutumia nafasi iliyopo kwenye miungano ya kibiashara kama COMESA na EACC kupenya katika masoko ya nje,” akasema kwenye hafla ya uteuzi wake. Balozi huyo ana tajriba mkubwa katika usimamizi wa bodi za kampuni mbalimbali.