Habari Mseto

Benki ya I&M yafungua tawi la Watamu

February 28th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

BENKI ya I&M inaendelea kutoa huduma za bure za kutoa pesa kutoka benki hadi kwa simu ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo kukuza biashara zao.

Aidha, imepunguza ada za mteja kutoa fedha katika akaunti yake ya benki.

Akizungumza Jumatano wakati wa ufunguzi wa tawi la I&M mjini Watamu, Kaunti ya Kilifi, meneja anayesimamia benki hiyo ukanda wa Pwani James Ng’ang’a amesema kwa sasa benki hiyo imebadili mfumo wake wa kuhudumia wananchi.

Maafisa wa I&M wakipiga picha pamoja baada ya ufunguzi wa tawi la Watamu mnamo Februari 28, 2024. PICHA | ALEX KALAMA

Dkt Ng’ang’a amesema benki hiyo inaangazia changamoto za mteja kama anavyojieleza anapofika katika benki hiyo kinyume na awali.

“Katika benki yetu, ukitaka kutoa pesa kutoka kwa akaunti yako hadi kwa simu yaani kwa njia ya M-Pesa hutozwi ada yoyote. Huduma hii unaipata bure kabisa,” akasema Dkt Ng’ang’a.

Kwa muda wa miezi miwili benki ya I&M imefungua matawi mawili, tawi moja likiwa mjini Kilifi na lile ambalo sasa limefunguliwa Watamu.

Meneja anayesimamia benki ya I&M ukanda wa Pwani James Ng’ang’a akihutubia wanahabari. PICHA | ALEX KALAMA