Habari Mseto

Benki ya Peter Kenneth yapata hasara ya mamilioni

August 30th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

WAKOPAJI kutolipa madeni na gharama ya juu ya kufanya biashara ni baadhi ya sababu zilizopelekea benki ya Mayfair inayohusishwa na mwanasiasa Peter Kenneth kupata hasara ya Sh76 milioni kati ya Januari na Juni mwaka huu.

Benki hiyo ilisema kuwa mapato yake baada ya gharama kuondolewa yalikuwa Sh49milioni, licha ya madeni kupanda hadi Sh1.26bilioni.

Kabla ya kuondoa gharama ya matumizi, benki hiyo ilitangaza mapato yake yalikuwa Sh129.9milioni.

Benki hiyo ilipewa leseni ya kutoa huduma za ukopeshaji pesa na benki kuu ya taifa (CBK) Juni mwaka jana, kipindi ambacho wateja wahifadhi Sh3.1bilioni nao.

Benki ya CBK ilisema kuingia kwa Mayfair sokoni kungepanua idadi ya benki ambazo Wakenya wanaweza kufikia na hivyo kuongeza ushindani.

Benki hiyo iliyo na matawi matatu hadi sasa ilisema inalenga soko la makampuni, huku ikiwa na matawi mawili Jijini Nairobi na la tatu Mombasa.

Hata hivyo, benki zingine zilishuhudia faid katika kipindi hicho, huku KSB ikitangaza asilimia 17.48 ya faida kutoka Sh12.1bilioni nayo benki ya Equity ikitangaza faida ya asilimia 17.52 hadi Sh11bilioni.

Benki ya Co-operative nayo iliangaza faida ya asilimia 7.57 katika kipindi hicho, huku Stanbic Holdings’ ikipokea Sh3.55bilioni kama faida.