Habari Mseto

Benki zasema kuna uhaba wa noti mpya nchini Kenya

July 13th, 2019 2 min read

Na PAUL WAFULA

BENKI za humu nchini zinakumbwa na uhaba wa noti mpya zilizozinduliwa Juni 2019 licha ya Benki Kuu ya Kenya kusema ilikuwa imesambaza pesa za kutosha.

Maafisa kadhaa wa benki, ambao waliomba majina yao yasitajwe, walisema walianza kukabiliwa na uhaba wa sarafu mpya wiki mbili baada ya kuikarabati mitambo yao ya kutoa na kuweka pesa (ATM).

Benki Kuu ya Kenya (CBK) imedinda kutoa maelezo kuhusu uhaba wa sarafu hizo mpya huku benki zikiendelea kuteseka na kuchanganyikiwa.

Kufuatia uhaba huo benki za humu nchini zimelazimika kurudia matumizi ya noti za zamani za Sh1,000 ambazo zimekuwa zikiondoa kutoka soko la fedha.

Shirikisho la Wanabenki Nchini (KBA) lilisema kutokana na hali hiyo, benki kadhaa zinakosa pesa za kuwakopesha wateja wao huku likiitaka CBK kutoa noti mpya za kutosha.

“Noti za zamani zingali halali na tutaendelea kuzitumia. Hakuna kinachozuia benki ambazo zinakumbwa na uhaba wa noti mpya kuendelea kutumia zile za zamani,” Mkurugenzi Mkuu wa KBA Habil Olaka aliambia Taifa Jumapili kwa simu.

“Natarajia kwamba changamoto hizo zitashughulikiwa haraka ili kuanzia miezi ya Agosti na Septemba benki zote zitakuwa zikipeana noti mpya,” alisema.

Uchunguzi umebaini kwamba benki zilizoko katika miji iliyoko mbali na Nairobi ndizo zimeathirika zaidi na uhaba wa sarafu mpya.

Wadau wengine katika sekta ya benki wanasema changamoto nyingine inayowakabili ni ukosefu wa mafunzo kuhusu masuala kadhaa kuhusu sarafu hizo mpya. Wanasema CBK ilianza kutoa mafunzo hayo wiki kadha baada ya kuzinduliwa kwa sarafu hizo mpya.

“Tunatumia mfumo wa kuwafundisha maafisa wetu wachache kwanza, na kisha kuwatuma kwenda kuwafunza wengine,” Bw Olaka alisema.

Hatua ya benki za kibiashara kurejelea matumizi ya noti za zamani ina maana kuwa zile noti ambazo zilikuwa zimeondolewa kutoka kwa soko la fedha zinarejeshwa tena. Hali hii inafanya mpango wa kuondoa noti hizo za zamani kukosa manufaa yaliyokusudiwa.

Madaraka Dei

Mnamo Juni 1, 2019, wakati wa sherehe ya Madaraka Dei Gavana wa CBK Patrick Njoroge aliwashangaza Wakenya alipotangaza kuwa itaanza kuondoa noti za zamani za Sh1,000 na kusambaza mpya katika hatua ya kupambana na ufisadi na tabia ya watu kuhifadhi pesa nyumbani mwao.

Alitangaza kuwa kuanza Oktoba 1, mwaka huu, noti za zamani za Sh1,000 hazitatambuliwa kama pesa halali.

Baada ya tangazo hilo, benki za kibiashara zilianza kuikarabati mitambo yao ya ATM ili iweze kuanza kutoa noti mpya.

Ilitarajiwa kuwa baada ya benki hizo kukamilisha zoezi la kukarabati ATM hizo, zitaanza kutoa noti mpya ili kuharakisha mpango mzima wa kuondoa noti za zamani na kuzirejesha kwa CBK.

Nchini Kenya kuna mitambo 1,700 ya ATM, matawi 780 ya benki za kibiashara na maajenti 66,000 wa benki.

KBA ilitoa ushauri kwa benki, maajenti wa benki, wabadilishaji sarafu na wananchi kwa jumla kuwa waangalifu katika kipindi hiki cha mpito kwani watu wengine wanaweza kutakasa pesa za wizi kupitia mfumo wa benki.