BENSON MATHEKA: Manifesto hazifai kupandisha joto la kisiasa nchini sababu ni ahadi hewa

BENSON MATHEKA: Manifesto hazifai kupandisha joto la kisiasa nchini sababu ni ahadi hewa

NA BENSON MATHEKA

MDAHALO umezuka kuhusu manifesto za wagombeaji urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mdahalo huo unatarajiwa kuendelea huku uchaguzi mkuu ukikaribia. Sawa na wagombeaji urais, wanaogombea ugavana pia wana manifesto zao zinazovutia na kuzua mjadala katika kaunti zao.

Japo katika manifesto hizo wagombeaji hao wameahidi mengi mazuri, wapigakura wanafaa kujifunza kutokana na historia ya wanasiasa. Katika nchi hii, manifesto huwa ni chombo cha kuomba kura tu.

Lengo la kuahidi mazuri huwa ni kuvutia wapigakura wawachague kwenye uchaguzi mkuu.

Wakiingia mamlakani, viongozi huwa wanageuza fikira zao na kushughulikia maslahi yao ya kibinafsi huku wapigakura wakisubiri watimiziwe waliyoahidiwa katika manifesto zao.

Na kuhusu kusubiri huku, huwa wanasubiri hadi baada ya miaka mitano, wanasiasa wanaporudi mashinani kuomba kura tena.

Kwa kawaida, wanasiasa huwa wanaahidi wapigakura paradiso wakiingia mamlakani.

Kwa mfano, kwa wakati huu wagombeaji hao wanaahidi kupunguza gharama ya maisha lakini hawaelezi mbinu watakazotumia kubadilisha hali hii inayoshuhudiwa kote ulimwenguni.

Ajabu ni kwamba wapigakura, kwa sababu ya kupofushwa na ushabiki wao kwa wanasiasa wanaounga mkono, huwa hawatambui uongo ambao wagombeaji huwa wananakili katika manifesto zao.

Ukweli ni kwamba manifesto hizo ni maandishi yaliyojazwa kwenye karatasi kupumbaza wapigakura.

Wanasiasa wanapoingia uongozini, huwa wanalewa mamlaka na kuanza kuweka sera na kupitisha sheria za kukandamiza raia waliowachagua.

Maneno matamu ya kuvutia na kutia moyo huwa yanatoweka na kuchukuliwa na kauli za uhusiano mwema ili kuepuka ghadhabu ya raia wanaovunjika moyo kwa kutotimiziwa waliyoahidiwa katika manifesto.

Wanachofanya wanasiasa katika manifesto zao ni kuambia watu wanachotaka kusikia tu lakini sio kinachoweza kutekelezeka au wanachoweza kutekeleza. Hivyo basi, mdahalo kuhusu manifesto haufai kupandisha joto la kisiasa nchini.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Unga: Serikali imewasaliti raia kwa mfumuko...

Majeshi ya Urusi yateka mji mwingine Ukraine

T L