BENSON MATHEKA: Museveni amegeuza Uganda kuwa mali ya kibinafsi

BENSON MATHEKA: Museveni amegeuza Uganda kuwa mali ya kibinafsi

Na BENSON MATHEKA

UCHAGUZI wa urais wa wiki jana katika nchi jirani ya Uganda, una mafunzo mengi yanayoweza kuwazindua raia wa nchi hiyo na kuwakomboa kutoka minyororo ya utawala wa Rais Yoweri Museveni.

Kutokana na matukio ya kabla na baada ya uchaguzi huo ni wazi kwamba Museveni alijipatia miaka mingine mitano mamlakani baada ya kuhakikisha uchaguzi ulifanyika katika giza. Hii ni kwa sababu siku mbili kabla ya Januari 14, aliagiza serikali kuzima intaneti hatua ambayo ilififisha matumaini ya uwazi na haki katika uchaguzi huo.

Hapa ndipo kuna funzo la kwanza kwa raia wa nchi hiyo. Sio kwa sababu kuzima intaneti kulitia doa udilifu wa uchaguzi huo, mbali pia kuliwanyima mamilioni ya raia fursa ya kufanya kazi zao za kila siku.

Kuzima huduma za mitandao kulizima maisha ya raia wa Uganda kwa siku nne mfululizo kwa sababu shughuli za kikazi hazingeendelea enzi hizi ambazo biashara na huduma zinategemea intaneti.

Wanachopaswa kujifunza raia wa nchi hiyo na hasa wafuasi wa Museveni ni kwamba rais huyo hawajali kamwe, anawachukulia kuwa wajinga na watumwa wake.

Kama angekuwa anawajali, hangechukua hatua ambayo ingelemaza shughuli zao na kukatiza mawasiliano yao na maeneo mengine ulimwenguni.

Funzo la pili ambalo raia wa Uganda wakiwemo maafisa wa usalama ambao anaendelea kutumia kunyanyasa viongozi wa upinzani na wafuasi wao ni kwamba adui mkubwa wa Uganda ni Museveni na familia yake na sio viongozi wa upinzani au mataifa ya kigeni anayodai yanawafadhili.

Anachowafanya raia wa nchi hiyo kuamini ni kwamba ni yeye tu au watu wa familia yake wanaofaa kuongoza Uganda.Kwa wafuasi wa chama chake cha National Resistance Movement, viongozi wa upinzani ni maadui wao ingawa ukweli wa mambo ni kuwa kiongozi huyo ni sumu kwao nchi hiyo.

Ni wazi kuwa nchi hiyo imekuwa tulivu kwa miaka 36 ambayo amekuwa mamlakani lakini hatua yake ya kukwamilia mamlakani kupitia udaganyifu katika uchaguzi, inaiweka katika hatari kubwa atakapoondoka usukani.

Katika nchi ambayo asilimia 80 ya raia wake ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 30, Museveni anafaa kufahamu kuwa hatawakwamilia enzini milele.

Funzo la tatu ambalo raia wa Uganda wanafaa kufahamu ni kwamba Museveni anaweza kuwaacha waangamie huku akitangazia ulimwengu kwamba kila kitu ni shwari nchini humo. Hili lilijitokeza wazi serikali yake ilipowazuia wanahabari na wachunguzi wa kimataifa kufuatilia uchaguzi huo. Kiongozi asiyetaka uwazi ni hatari kwa raia wake.

Tano, raia wa Uganda wanafaa kufahamu bila chembe la shaka kuwa Museveni sio mwanademokrasia. Anachoita uchaguzi nchini humo ni mbinu ya kuwataka raia kuidhinisha uongozi wake wa kiimla na kwa kuwa huwa wanakataa kufanya hivyo, huwa anatumia udaganyifu na vitisho.

Hakuna demokrasia katika nchi ambayo wanajeshi hutumiwa kutisha na kuhangaisha upinzani na raia. Ukweli usioweza kupingwa ni kwamba alianza vyema alipoingia mamlakani 1986 lakini anayetawala kwa wakati huu sio Museveni aliyekosoa marais wanaokwamilia mamlakani. Kwa sasa, Uganda ni mali yake, na raia ni watumwa wake.

You can share this post!

Wanamuziki wajiandaa kuvuna vinono siasa za 2022 zikinoga

MAUYA OMAUYA: Bobi Wine ameweka msingi, mapambazuko...