BENSON MATHEKA: Serikali haifai kupuuza ripoti ya Human Rights Watch

BENSON MATHEKA: Serikali haifai kupuuza ripoti ya Human Rights Watch

Na BENSON MATHEKA

Ripoti ya shirika la Human Rights Watch iliyofichua kwamba Sh10 bilioni ambazo serikali ilisema zilitumiwa kusaidia watu maskini kukabiliana na makali ya corona zilinufaisha machifu, jamaa zao na za maafisa wakuu serikalini inaonyesha kiwango cha uozo wa ufisadi nchini.

Serikali ilitangaza msaada huo mwaka jana ilipoweka kanuni kali za kuzuia msambao wa virusi vya corona zilizoathiri uchumi.

Ilisema kwamba pesa hizo zingetumiwa kukinga maskini waliokuwa hatarini hasa katika mitaa ya mabanda mijini.

Kulingana na ripoti hiyo, pesa hizo zilifikia asilimia 4.8 pekee ya waliolengwa kunufaika, kumaanisha nyingi ziliporwa au kuelekezwa kwa watu ambao hawakufaa kuzipata.

Kwa kuwa serikali ilikanusha ripoti hiyo licha ya ushahidi kukusanywa kutoka mashinani, inawezekana kuwa ilidanganya ilikuwa imejitolea kusaidia maskini kukabiliana na makali ya janga la corona ilhali iliwaacha wateseke.

Kwa kila hali, ripoti hiyo inafichua jinsi maafisa wakuu serikalini wanavyotumia raia kupora mali ya umma.

Inaanika wazi mbinu chafu ambazo maafisa wa serikali hutumia kuficha ufisadi wakisingizia wanalenga kusaidia akina yahe.

Sio mbinu geni kwa kuwa imekuwa ikifanya hivi kila wakati mara mikasa au majanga yanapotokea.

Inatumia hali ya ukame na mafuriko kutenga na kuomba misaada ya mabilioni ya pesa ambazo huwa zinaporwa huku waathiriwa wakiendelea kuteseka na hata kufariki.

Sio mara moja serikali imetoa pesa kununua chakula cha misaada ambacho hakifikii wakazi wanaokihitaji huku ripoti za uhasibu zikionyesha mabilioni yalitumika.

Kwa maafisa wa serikali wanaopata mshahara kila mwezi kutoka kwa ushuru unaotozwa umma na kisha kunufaika na pesa zinazotengwa kusaidia wakazi wanapoathiriwa na janga ni kilele cha ukosefu wa utu.

Badala ya kukanusha ripoti ya Human Right Watch, serikali ingeitumia kubaini makosa yalivyotokea, waliohusika na washirika wao.

Kukanusha haraka bila kubainisha ukweli kunaonyesha kuwa kuna kitu ambacho serikali au maafisa wake waliohusika wanataka kuficha.

Kufanya hivi ni kufunika kidonda kinachotoa usaha kwa kitambaa chepesi.Hii ndio sababu imekuwa vigumu kukomesha ufisadi humu nchini kwa kuwa wanaopaswa kufanya hivyo ndio huwa msitari wa mbele kuuficha, kuutekeleza au kukinga wahusika.

Wakifaulu kuuficha huwa wanasubiri kwa hamu janga jingine litokee walitumie kupora mabilioni zaidi kujilimbikizia utajiri huku wanaosingizia kusaidia wakiteseka.

Hivi ndivyo ilivyoshuhudiwa katika kashfa ya mabilioni yaliyotengwa kukabiliana na janga la corona. Huu ndio ukweli uliofanya maafisa wa serikali kukanusha ripoti ya Human Right Watch.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Raia wanabaguliwa katika utekelezaji...

Sera ya wajawazito kuingia darasani ifutwe, walimu warai