BENSON MATHEKA: Serikali iweke mikakati ya kulinda wakulima dhidi ya ukosefu wa mvua

BENSON MATHEKA: Serikali iweke mikakati ya kulinda wakulima dhidi ya ukosefu wa mvua

NA BENSON MATHEKA

KILA hali inaonyesha kuwa mvua inayotarajiwa nchini kuanzia mwezi Oktoba haitakuwa ya kutosha kama ilivyoshauri idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini.

Idara hiyo imeshirikiana na mashirika mengine ya kimataifa kuonya kuwa sehemu nyingi nchini hazitapata mvua ya kutosha.

Baada ya idara hiyo kutekeleza jukumu lake la kutahadharisha kuhusu hali ya mvua itakavyokuwa, ni jukumu la serikali kupitia idara zinazohusika kujiandaa kuepushia raia madhara yanayotokana na ukosefu wa mvua ya kutosha.

Maandalizi haya yanafaa kuwa ya kuweka mikakati ya kuepusha raia na baa la njaa linalonukia. Hii ni kwa sababu utakuwa msimu wa tano mvua kukosa kunyesha katika baadhi ya maeneo hasa ya Kaskazini, Kaskazini Mashariki na Kusini Mashariki.

Hakuna haja ya wakulima ambao wako na ari ya kupata chakula kupanda mbegu ambazo hazitawapa mavuno kwa sababu ya kukosa mvua ya kutosha.

Kufanya hivyo ni kujiongezea hasara wakati ambao wanakabiliana na hali ngumu ya maisha.

Hivyo basi, maafisa wa wizara ya afya na wataalamu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo nchini (KALRO), wanafaa kuwashauri wakulima aina ya mbegu na mimea wanayopaswa kupanda ili kupata mavuno mema.

Maafisa wa kilimo wanafaa kuwaepushia hasara kwa kuwapa ushauri unaofaa.

Kwa kutekeleza jukumu lake la kuhakishia raia utoshelevu wa chakula hata katika nyakati hizi ambazo ulimwengu unakabiliana na mabadiliko ya tabianchi, serikali inafaa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zinazofaa kwa kila eneo kwa msimu huu, na mbolea ya kutosha.

Ikichukua hatua hizi, madhara yanayotokana na uhaba wa mvua na tishio kwa utoshelevu wa chakula yatapungua.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali itumie busara kuhusu suala kuu la...

Ebola: Uganda yaripoti maambukizi, vifo zaidi

T L