Makala

BENSON MATHEKA: Tuchunge utapia mlo usiwe janga la taifa

November 11th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Ripoti kwamba idadi ya watoto wanaosumbuliwa na utapia mlo imeongezeka maeneo tofauti nchini inatia wasiwasi.

Hii inaonyesha kuwa utapia mlo unaweza kuwa janga katika taifa hili ikiwa hatua hazitachukuliwa kurekebisha hali kwa kuhakikisha kuwa watoto wanapata lishe bora.

Kufanya hivi kutahitaji sera thabiti ya kiuchumi ili kuhakikisha kila Mkenya ana uwezo wa kujipatia riziki.Sababu ya kusema kuwa utapia mlo unaweza kuwa janga la kitaifa, ni kwamba licha ya kiwango cha hali hii kuwa cha juu nchini, serikali haijaonyesha kujitolea kuikabili. Kulingana na Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto (UNICEF), kiwango cha Wakenya wanaotatizwa na utapia mlo kimefikia asilimia 27.

Shirika hili linasema kwamba kiwango cha utapia mlo katika nchi kinapozidi asilimia 25, hali ya hatari huwa inabisha hodi. Ingawa UNICEF inasema kwamba Kenya inafanya juhudi za kupongezwa za kukabiliana na hali hii, huenda hatua zilizopigwa zikivurugwa na athari za janga la corona baada ya mamilioni ya Wakenya kupoteza mbinu za kujipatia mapato.

Itakumbukwa kwamba kabla ya corona kuripotiwa nchini watoto wengi katika maeneo kame walikuwa wakipatiwa chakula shuleni na si ajabu wanateseka kwa miezi tisa ambayo shule zimefungwa.

Serikali haikuweka mikakati ya kufuatilia kubaini hali ya watoto hao na hata shule zitakapofunguliwa Januari, huenda ikawa vigumu kuwapatia chakula shuleni kwa sababu ya kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi hivi.

Kuna haja ya wizara ya elimu na serikali za kaunti kubuni mikakati ya kulinda watoto dhidi ya utapia mlo ili kuhakikisha nchi itakuwa na raia wenye afya siku zijazo.

Serikali za kaunti zina uwezo wa kuhamasisha wakazi kuhusu mbinu za kuimarisha lishe, kutambua na kusaidia wanaolemewa na hali hii hasa wakati wa kiangazi.

Hili linawezekana kwa kutenga pesa katika bajeti kila mwaka ambazo zitatumiwa kwa shughuli hii na kama zipo, zisitumiwe vibaya au kuelekezwa kwa mipango tofauti.

Kwa kufanya hivi, vifo vinavyotokana na utapia mlo vitaepukwa na nchi kuwa na raia wenye afya. Inahuzunisha kuona watoto waliodhoofika kiafya kando ya wazazi ambao hawana uwezo wa kuwalisha wakati kuna serikali inayofaa kuweka mikakati ya kuimarisha maisha yao.

Inasikitisha kuona wazee wakifa njaa wakati wa kiangazi ilhali kuna idara ya serikali inayotengewa pesa za kukabiliana na hali hii.

Serikali za kaunti zinafaa kuwa msitari wa mbele kulinda watoto ilivyokuwa ikifanyika miaka ya sabini na themanini ambapo maafisa wa afya walikuwa wakitembea vijijini kuwaelimisha wazazi kuhusu jinsi ya kutunza afya za watoto.

Kwa kuimarisha uchumi ili kila mmoja apate riziki ya kila siku, hali hii inaweza kuepukwa. Taifa haliwezi kuwa na jamii yenye afya bora ikiwa watoto watakosa kukua vyema kwa kukosa lishe bora.

Ikiwa hilo lilikuwa likitendeka nyakati hizo wakati ambao hakukuwa na ugatuzi, linaweza kutendeka wakati huu kukiwa na nia njema.